M/Kiti CCM apewa kongole kuchagua safu makini ya madiwani
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya
Dodoma amepongezwa kwa kupanga safu makini ya wagombea nafasi ya udiwani jambo
lililowawezesha kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipotoa salamu katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Alhaj Shekimweri alisema “nichukue nafasi hii
kuwapongeza waheshimiwa madiwani kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa madiwani kwa
kata zenu, ninyi mnatokana na CCM. Mstahiki Meya, nichukue nafasi hii
kumpongeza Mwenyekiti, Charles Mamba kwa kuteua madiwani wazuri waliofanya
kampeni zao kistaarabu na kuchaguliwa kwa kishindo kuunda Baraza la Madiwani la
Jiji la Dodoma”.
Aidha, aliwapongeza wabunge wa Jimbo la Dodoma Mjini
na Mtumba kwa kuchaguliwa kuwa wabunge. “Mstahiki Meya, ulikuwa ni Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani, nichukue nafasi hii kuwapongeza wabunge wetu,
Mheshimiwa Chinyele na Mheshimiwa Mavunde pamoja na wale wa viti maalum wote.
Wameshimiwa wabunge hongereni kwa kinyang’anyiro na hongereni kwa kuwa Madiwani
wa Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma. Lakini pia, ulikuwa uchaguzi wa rais
tunampongeza kwa dhati Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae alipata ushindi wa
kishindo wa karibu asilimia 97.7 na kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania” alisema Alhaj Shekimweri.
Katika hatua nyingine, Mstahiki Meya Jiji la Dodoma,
Alimwoni Chaula alishukuru kwa kuchaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma
na kuahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na baraza la madiwani ili kuongeza
kasi ya maendeleo kwa wananchi.
Alisema kuwa vipo vipaumbele muhimu atakavyoanza navyo
katika kuhakikisha jiji linasonga mbele. “Vipo vipaumbele muhimu kama vile
kusimamia masuala ya ardhi, kusimamia mapato, mikopo ile ya makundi maalum
tunaelewa tuna vijana ambao wanahitaji kukuza uchumi wao binafsi. Kuna masuala
ya elimu na maji, vyote hivyo tutaenda kuvisimamia kwa weledi mkubwa” alisema
Chaula.
Nae, Diwani wa Kata ya Madukani, Prof. Davis Mwamfupe
alisema kuwa anawapongeza madiwani wenzake kwa kufanikisha uundaji wa Baraza
jipya la Madiwani. “Natoa pongezi kwetu sote, nina imani baraza hili litakwenda
kuwa bora na la kipekee kwasababu unaona idadi kubwa ya waliochaguliwa ni
vijana. Vijana wana nguvu, ari na mwamko wa kuchapa kazi” alisema Prof.
Mwamfupe.
MWISHO
Comments
Post a Comment