DC Shekimweri asisitiza semina elekezi kwa madiwani Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri
amesema kuwa semina elekezi kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni
muhimu ili kuwapa maarifa na kufanya uendeshaji wa mikutano ya halmashauri kuwa
ya viwango kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiwasalimia madiwani katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma baada ya Uchanguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa tarehe 29 Oktoba, 2025.
“Ninawapongeza kwa dhati Mstahiki Meya, Chaula na
Naibu Meya, Fundikira kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na baraza hili. Ninyi
bado ni vijana, kwa hiyo baraza hili lina sura ya viongozi wa vijana.
Ukiangalia waheshimiwa madiwani wengi pia ni vijana, hapo peke yake ni fursa
lakini pia ni changamoto msipoangalia vizuri. Nami niungane na mtoa hoja wa
kwanza, kwamba yakaandaliwa mafunzo na kupata semina elekezi ili msheheni
maarifa, uelewa wa taratibu za vikao, lakini kanuni za kudumu za Baraza la
Madiwani. Kwa sababu katika mkutano huu mara zote ni kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu na miongozo ya nchi, siyo nje ya hapo. Dunia ya leo maarifa
yanapatikana kwa njia nyingi na rafiki, njia nyepesi ya kwanza wapo madiwani
wazoefu na wengine wana vipindi viwili hadi vitatu. Mpo na Mstahiki Meya
Mstaafu Prof. Mwamfupe na wengine wanaweza kushea. Lakini maarifa mengine yapo
kwenye mtandao tu, nina fahamu kuna utaratibu wa kuwapatia vishikwambi kwa
ajili ya uratibu wa vikao na taarifa za vikao. Mnaweza kuwawekea nyaraka hizo
wakaanza kuzisoma taratibu. Nasema haya kwa sababu mnabeba matajio makubwa ya
wakazi wa Dodoma” alisema Alhaj Shekimweri.
Aliwataarifu kuwa matarajio ya wananchi ni kuona kasi
ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, utendaji wa jiji na utoaji wa huduma
bora ikiongezeka. “Nawapongeza wote mliochaguliwa kuwa wenyeviti wa kamati za
kudumu pamoja na wajumbe, kazi nyingi zitaanzia kwenye kamati zetu. Tunategemea
kupata huduma bora kwenye sekta za afya, elimu, umeme, maji barabara, yote haya
wananchi wanawaangalia ninyi. Nendeni mkatekeleze kwa kuzingatia Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya Mwaka, 2025-2030” alisema Alhaj Shekimweri.
MWISHO
Comments
Post a Comment