Waziri Mavunde akabidhi vifaa vya Michezo UMISETA Dodoma

 

Na. Mwandishi wetu, DODOMA


Wanafunzi wanaojiandaa kushiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) ngazi ya mkoa wamepata hamasa mpya baada ya kupokea vifaa vya michezo vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.




Vifaa hivyo vilikabidhiwa katika Shule ya Sekondari Dodoma kwa niaba ya Mbunge huyo kupitia Katibu wake, Silas Makanyaga, ambae alisema kuwa Jiji la Dodoma kupitia Ofisi ya Afisa Elimu Sekondari liliwasilisha ombi la vifaa vya michezo kwa ajili ya mashindano ya UMMISETA ngazi ya wilaya na mkoa, ambapo Mbunge amejitoa kusaidia kwa kununua jezi kwa kila mchezo.

“Tunawaomba vijana wetu kucheza kwa nidhamu, kuwasikiliza walimu wao na kuendelea kufanya vizuri kama ilivyo desturi ya Jiji la Dodoma ambalo limeendelea kuwa kinara kwa ushindi wa makombe mbalimbali” alisema Makanyaga.

Kwa upande, Afisa Elimu Sekondari Jiji la Dodoma, Mwl. Daniel Mapilya alisema kuwa tayari wanafunzi 120 kutoka shule mbalimbali za sekondari wamewasili kambini tangu Juni 5 kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya ngazi ya mkoa yaliyotarajiwa kuanza rasmi Juni 8 mwaka huu. 

 



“Vijana hao wameonyesha utayari mkubwa wa kushiriki na kuonesha ushindani wa hali ya juu. Tumepokea vifaa mbalimbali ikiwemo jezi ambazo zimeongeza ari na furaha kwa wanafunzi wetu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kusimama nasi na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo” alisema Mwl. Mapilya.

Sambamba na hilo, Afisa Michezo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Peter Ititi alisema kuwa vifaa vilivyotolewa vimeongeza morali na hamasa kwa wanamichezo, akibainisha kuwa kwa miaka minne mfululizo mbunge huyo amekuwa akiwaunga mkono kwa kutoa vifaa vya michezo jambo lililosaidia kuongeza ushindani na mafanikio.

Nae, mchezaji wa mchezo wa kurusha tufe na Mpira wa Pete, Munira Mohamed alisema kuwa vifaa walivyopokea kutoka kwa mbunge vimeongeza hamasa na kuwapa nguvu ya kupambana kwa ushindi.

Hata hivyo, Nahodha wa timu ya mpira wa miguu, Gabriel Peter alisema kuwa timu ipo katika maandalizi mazuri na watapeperusha vizuri bendera ya Jiji la Dodoma kwa kurudi na ushindi mnono wa makombe kama zawadi ya shukurani kwa mbunge.

Mashindano ya UMISETA ngazi ya mkoa kwa Jiji la Dodoma yanashirikisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu (football), mpira wa pete (Netball), mpira wa kikapu (Basketball), mpira wa mikono (Handball), mpira wa wavu (Volleyball), riadha, sanaa za ndani, muziki wa kizazi kipya, tenisi ya mezani (Table Tennis), Goalball, kwaya na ngoma za asili.

 

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026