Vita dhidi ya Mbegu feki vyazaa matunda

Na. Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma


Serikali imeendelea kuimarisha hatua za kudhibiti na kutokomeza tatizo la mbegu feki nchini kupitia mifumo ya kisasa ya uthibitishaji wa ubora, ukaguzi wa mara kwa mara na utoaji wa elimu kwa wakulima.




Akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Onesmo Merdson Mnkondya, kuhusu mpango wa Serikali wa kukomesha mbegu feki nchini, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 15 cha Sheria ya Mbegu (Sura ya 308, Toleo la Urekebu la mwaka 2023), mbegu zote zinazouzwa nchini zinapaswa kuthibitishwa ubora wake na Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI).

Silinde aliaema kuwa TOSCI imeanzisha matumizi ya lebo za kielektroniki zinazotolewa kwa kampuni za mbegu ili kuwasaidia wakulima kuhakiki uhalisia wa mbegu wanazonunua. Kupitia mfumo huo, mkulima anaweza kukwangua lebo maalum iliyowekwa kwenye kifungashio cha mbegu na kuingiza namba husika kwenye simu yake ya mkononi ili kupata taarifa za uthibitisho wa mbegu hizo.

Matumizi ya teknolojia hiyo yameleta mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya mbegu feki, ambapo matukio yaliyoripotiwa yamepungua kutoka 325 mwaka 2014/2015 hadi kufikia matukio 10 pekee mwaka 2023/2024.

Mbali na matumizi ya teknolojia, serikali kupitia TOSCI inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka yanayouza mbegu nchini. Katika ukaguzi uliofanyika kati ya Julai 2025 na Januari 2026, wafanyabiashara 13 walibainika kujihusisha na uuzaji wa mbegu feki au mbegu zisizokidhi viwango vya ubora.

Kwa mujibu wa waziri, kesi moja tayari ipo mahakamani huku uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wengine 12 ukiendelea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora na namna ya kutambua mbegu feki. Kupitia Kampeni ya Mali Shambani, wakulima 5,822 walipatiwa elimu hiyo, huku wakulima wengine 6,763 wakipata huduma na ushauri kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Center) katika kipindi cha Novemba 2025 hadi Januari 18, 2026.

Silinde alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya mbegu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na salama, sambamba na kuwalinda dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu feki.

 

Chanzo: Michuzi Blog

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026