Wanawake watakiwa kulipa kodi na kukuza uchumi katika Jiji la Dodoma
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Wanawake
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, hususan wafanyabiashara na wajasiriamali,
wametakiwa kuendelea kulipa kodi na tozo kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya
jiji pamoja na kukuza uchumi wao na wa jamii kwa ujumla.
Wito huo ulitolewa na Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Zuzu, Pilly Hassan, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 8 Machi, 2026.
Alisema
kuwa ulipaji wa kodi ni moja ya njia muhimu inayosaidia serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo ikiwemo kuboresha miundombinu ya masoko, barabara na huduma
nyingine muhimu kwa wananchi. “Wanawake wengi wa Jiji la Dodoma tunajishughulisha
na shughuli za biashara na ujasiriamali. Hivyo, tunapaswa kuwa mfano mzuri kwa
kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu wa kulipa kodi na tozo za serikali kwa hiari
na kwa wakati. Kupitia kodi hii itaweza kutusaidia mambo mbalimbali na ya
muhimu kama vile kujenga shule, masoko, barabara, hospitali na huduma nyingine.
Hivyo, tunapaswa kuwa mstari wa mbele zaidi kuhakikisha jiji letu linakuwa
kiuchumi kupitia mapato yetu” alisema Hassan.
Pia
aliongeza kwa kusema “wanawake tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia
maendeleo ya jiji letu. Kupitia ulipaji wa kodi, tunasaidia kuimarisha uchumi
wa jiji na pia kuendeleza biashara zetu na tuhakikishe tunahamasishana sisi kwa
sisi katiia suala zima la ulipaji wa kodi” alisema Hassan.
Kwa
upande wake, Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Dodoma Mjini, Flora Liacho
alisema kuwa wanawake wanapaswa kushirikiana na serikali katika nyanja mbalimbali.
“Tunapaswa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuibua fursa za kiuchumi
pamoja na kuwahamasishana wanawake kujiunga katika shughuli za ujasiriamali
zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi” alisema Liacho.
Lakini pia alitoa wito wanawake wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2026 ambapo kimkoa yatafanyika katika Wilaya ya Kongwa. “Nichukue fursa hii kuwataka wanawake wenzangu tuungane kwa pamoja katika siku yetu ya wanawake tujumuike kwenda kusheherekea katika Wilaya ya Kongwa, kuna vitu vingi vya kujifunza kama vile masuala ya ujasiliamali, haki kwa mwanamke na vitu vingine vingi. Hivyo, wanawake tujumuike kwa pamoja katika siku yetu” alisema Liacho.
Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 8 Machi na hulenga
kuenzi mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii pamoja na kuhimiza usawa wa
kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kijamii. Kwa mwaka 2026 Mkoa wa
Dodoma unaadhimisha siku hiyo katika Wilaya ya Kongwa chini ya kaulimbiu isemayo
“Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050”.
Comments
Post a Comment