Wawezeshaji Stadi za Maisha watakiwa kuwa na nidhamu na uwajibikaji

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Wawezeshaji wa Stadi za Maisha katika Shule za Sekondari Jiji la Dodoma wametakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika mazingira ya shule watakazopangiwa pamoja na kutumia mafunzo waliyoyapata kwa kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi.



Hayo yalisemwa na Mwezeshaji mafunzo ya Stadi za Maisha wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Tuvacal Mjema, wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dodoma jijini Dodoma.

Alisema kuwa wawezeshaji wanapaswa kuwa mfano bora kwa wanafunzi kwa kuzingatia maadili, kuwajibika ipasavyo na kuonyesha weledi katika utekelezaji wa majukumu yao. “Ni muhimu kwa wawezeshaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu wanapokuwa shuleni. Tunapaswa kuishi yale tunayowafundisha wanafunzi ili waweze kutuamini na kufuata miongozo tunayowapatia kwasababu ninyi ndio taa yao  inayo waangazia” alisema Mjema.

Lakini pia aliongezea kwa kusema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea uwezo wa kitaaluma na kisaikolojia wawezeshaji ili waweze kuwasaidia wanafunzi. “Kupitia mafunzo haya ninaamini kuwa tunawaongezea walimu ujuzi ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za wanafunzi zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku na masomo kwa ujumla” alisema Mjema.



Kwa upande wake, Sophia Kasekwa ambaye ni Mwezeshaji wa Stadi za Maisha katika Shule ya Sekondari Miyuji, alisema kuwa kupitia mafunzo hayo wamepata maarifa na mbinu zitakazowawezesha kuwafikia wanafunzi kwa ufanisi zaidi. “Tunashukuru kwa fursa hii ya mafunzo. Yametupa mwanga mpana wa namna ya kuwasaidia wanafunzi, hasa wale wenye changamoto mbalimbali za kimaadili, kisaikolojia na kijamii. Pia, kupitia elimu ya stadi za maisha, wanafunzi watajengewa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujiamini na kukabiliana na shinikizo rika, hali itakayochangia kuboresha taaluma na mwenendo wao shuleni na katika jamii kwa ujumla” alisema Kasekwa.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika Shule za Sekondari jijini Dodoma, lakini pia kuwajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na mitazamo chanya itakayowawezesha kujitambua, kujiamini, kufanya maamuzi sahihi na kukabiliana kwa ufanisi na changamoto za maisha ya kila siku, ili waweze kuwa raia wenye maadili mema, uwajibikaji na mchango chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Dodoma English Medium kusomesha kwa gharama nafuu

Ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu wafikia 98%

Ujenzi wa Darasa Sekondari Anthony Mavunde kupunguza msongamano kwa wanafunzi