Stadi za Maisha Kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa Sekondari jijini Dodoma

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Elimu ya Stadi ya Maisha imetajwa kuwa ni chachu ya mabadiliko chanya kwa wanafunzi katika kuwajengea uwezo wa kujitambua na kukabiliana na changamoto za maisha katika shule za sekondari jijini Dodoma.



Hayo aliyasema Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Daniel Mapilya wakati akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa stadi za maisha katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dodoma.

Alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wawezeshaji wanapata uelewa wa kutosha juu ya namna bora ya kuwafikia wanafunzi na kuwajengea misingi imara ya maisha. “Tunapozungumzia stadi za maisha, tunalenga kumsaidia mwanafunzi kujitambua, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi. Elimu hii itawawezesha vijana wetu kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuathiri masomo na mustakabali wa maisha yao” alisema Mapilya.

Aliongeza kwa kusema kuwa changamoto nyingi zimekuwa zikiwakumba watoto wa kike. ”…zikiwemo shinikizo la rika na mazingira yasiyo rafiki, hivyo elimu hiyo itawapa ujasiri wa kusimamia ndoto zao na kupambana na hali yoyote inayoweza kuwakwamisha, na kuweza kuwajengea wanafunzi uwezo wa kusema hapana na kusimamia maamuzi yao ni sehemu muhimu ya kuwapa kinga dhidi ya changamoto za kijamii” alisema Mapilya.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Lauden Emanuel, alisema kuwa mafunzo ya stadi za maisha ni nyenzo muhimu katika kumlea kijana mwenye malengo na maadili. “Tunataka kuona wanafunzi wanajijengea uwezo wa kufikia ndoto zao. Kupitia stadi za maisha, tutawasaidia hasa wanafunzi wa kike kujiamini, kujitambua na kusimama imara katika kufanikisha malengo yao ya elimu na maisha kwa ujumla. Kupitia mafunzo haya wanafunzi watajifunza namna ya kupanga malengo yao, kuyafuatilia na kuyatimiza kwa nidhamu na bidii” alisema Emanuel.



Wawezeshaji waliopatiwa mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa daraja muhimu la kufikisha maarifa kwa wanafunzi, hatua itakayosaidia kuongeza ufaulu, kuimarisha nidhamu na kujenga kizazi chenye maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Dodoma English Medium kusomesha kwa gharama nafuu

Ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu wafikia 98%

Ujenzi wa Darasa Sekondari Anthony Mavunde kupunguza msongamano kwa wanafunzi