Utatuzi mgogoro wa Mahomanyika watangazwa


Na. Nancy Kivuyo, NZUGUNI

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeunda timu mbili ya wataalam wa upangaji na upimaji na timu ya uhakiki kwaajili ya kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu katika eneo la Mahomanyika.


Timu hizo zimeundwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Mahomanyika, Kata ya Nzuguni jijini Dodoma.

Alisema kuwa timu hizo zitaanza kazi mara moja ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati. “Eneo la Mahomanyika ni la serikali kwahiyo, naagiza lipangwe na kupimwa kwaajili ya kutatua mgogoro huu na kuwa kielelezo cha utatuzi wa migogoro mingine iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma. Timu hizi zinapaswa kufanya kazi ndani ya siku 60 na kukamilisha zoezi hili ili kila mmoja ajue amepata nini na anaenda wapi” alisema Dkt. Akwilapo.

Aliongeza kuwa wale wote waliohusika kwenye kadhia ya mgogoro huo wa ardhi watachukuliwa kwaajili ya mahojiano ili wakatoe maelezo ya kina ya kuwezesha suluhu kupatikana. “Wale wote ambao kwa namna moja au nyingine walihusika kwenye kadhia hiyo watatafutwa na watahojiwa ili sasa watoe maelezo yatakayosaidia kupatikana suluhu ya mgogoro kwasababu tunataka suala hili liishe na maisha mengine yaendelee” aliongeza Dkt. Akwilapo.


Alimalizia kwa kutoa rai kwa viongozi wa ngazi zote za mitaa, kata na vitongoji kutambua kuwa masuala ya ardhi yanahitaji utaalam na nidhamu huku akikemea tabia ya viongozi kujifanya wamiliki wa ardhi na kusisitiza kuwa ili nchi iendelee, inahitaji mambo manne ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora na kwamba uongozi bora unajumuisha weledi katika kusimamia ardhi.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Nzuguni, Leonard Ndama, aliushukuru ujio wa waziri na timu yake akisema kuwa anatarajia mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu utamalizwa na hatimae wananchi kupata kile wanachostahili. “Nakushukuru sana Mheshimiwa waziri na jopo lote hili kwa kufika hapa Mahomanyika, ninaamini ya kuwa ujio wenu ni kusudi tosha la kupata majibu ya mgogoro huu na kufikia tamati kwa changamoto hii kutatuliwa” alisema Ndama.

Mgogoro huo unahusisha Mtaa wa Mahomanyika (Kata ya Nzuguni) na Mitaa ya Azimio na Sokoine (Kata ya Ipala) ambapo eneo lenye mgogoro lina jumla ya ekari 4,363. Hapo awali, mwaka 1976 eneo hilo lilipangwa kuwa "Green Belt" yaani Ukanda wa Kijani. Mpango wa mwaka 2019-2040 ulibadilisha matumizi hayo kuwa "Urban Farming" yaani Mashamba ya Mjini ambapo mwaka 2022, Jiji la Dodoma lilipanga viwanja 1,990 katika eneo hilo, hali iliyozua malalamiko kutoka kwa wananchi waliodai kuwa wamiliki wa asili.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Dodoma English Medium kusomesha kwa gharama nafuu

Ujenzi wa Kituo cha Afya Zuzu wafikia 98%

Ujenzi wa Darasa Sekondari Anthony Mavunde kupunguza msongamano kwa wanafunzi