Watumishi Bonanza lafana Jiji la Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Maelfu ya watumishi wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma wajitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri kushiriki Bonanza la
kuaga na kukaribisha mwaka mpya 2025.
Akizungumza wakati wa Bonanza hilo,
Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje, alisema kuwa, katika utumishi wake wa
miaka kumi hajawahi kuona bonanza la namna hiyo kuwahi tokea na alitumia nafasi
hiyo kumshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa kuwakutanisha watumishi wote kwa lengo
la kuimarisha mahusiano bora katika utendaji kazi. “Mimi nina mwaka wa 10
katika udiwani, toka nimekuwa Diwani halijawahi kutokea bonanza kama hili.
Nadhani niseme hili bila kuficha, kiongozi wa halmashauri kwa maana ya mkurugenzi,
ana upeo mkubwa sana kwa watumishi wake” alisema Maboje.
Kuhusu masuala ya mahusiano mema katika
utendaji na uboreshaji wa kazi, alisema, kukutanishwa kwa watumishi hao
kunajenga msingi bora wa maelewano na mshikamano. Maboje alisema “bonanza
hili linaonesha namna ambavyo Mkurugenzi ana mahusiano mazuri na watumishi anaowaongoza,
kwa kufanya hiki kitu kinajenga msingi wa maelewano na mshikamano. Maana yake
kama mtumishi anapoambiwa kuna majukumu fulani, atakuwa anakumbuka kuwa mimi nimeshafanyiwa
kitu hiki kwamba mkurugenzi anatujali. Kwahiyo, ninataka kusema kuwa, hii hapa
ni tija katika ufanisi wetu wa kazi na kufanya kazi kama timu”.
Aidha, alitoa wito kwa watumishi
waliohudhuria Bonanza hilo kuendelea kudumisha mshikamano waliouonesha na
kuufanyia kazi katika utoaji huduma kwa jamii. “Natoa wito kwa watumishi,
mshikamano waliouonesha leo, uendelee na hata katika kutoa huduma kwa jamii na
idara zote. Hili jambo la leo mkurugenzi na menejimenti yake wameonesha wema
wao kwa kutujali watumishi wa ngazi zote. Kwahiyo, nawaomba watumishi na
madiwani wenzangu tufanye kazi kwa mshikamano na kwa ushirikiano mkubwa ili
tuiinue halmashauri yetu na izidi kupanda” alitoa wito Maboje.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya
Mtumba, Hassan Kadoke, alipongeza bonanza hilo kwasababu limewakutanisha
watumishi mbalimbali na kufahamiana pia limeshirikisha michezo mbalimbali
iliyolenga kuimarisha na kuboresha afya. “Siku ya leo imekuwa nzuri kwetu
sisi watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kupitia maandalizi mazuri
aliyoyafanya Mkurugenzi wa Jiji kuandaa bonanza la kutukutanisha sisi watumishi
wa serikali. Kikubwa katika hili Bonanza tunachofurahi ni kwamba, limekutanisha
watumishi wote na idara mbalimbali, kwanza, kuja kufurahi na pili kufahamiana
kwasababu kuna baadhi ya idara hatufahamiani, watumishi kwa watumishi
hatufahamiani. Kwahiyo, limetukusanya watumishi wote na tumeweza kufahamiana”
alipongeza Kadoke.
Nae, Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma,
Peter Ititi, alishiriki mashindano ya Mchezo wa Drafti na kuibuka kidedea
katika fainali za mchezo huo ambapo awamu ya kwanza aliibuka mshindi. “Nimejipanga,
nimejifua wiki nzima nikijiandaa kushinda Mchezo wa Drafti na mpaka sasa mchezo
wangu wa kwanza nimeshinda. Kwahiyo, ninasubiri mshindi wa mchezo wa pili ili
nicheze nae. Nina hakika kombe hili ni la kwangu na lazima niwe mshindi wa
kwanza kwa vyovyote vile” alisema Ititi.
Bonanza lilifana kwa kuanza na mbio za
taratibu ‘jogging’ na kufuatia na michezo na burudani mbalimbali
zilizopendezesha tamasha hilo kama mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba,
mchezo wa bao, drafti, kukimbiza kuku na burudani na muziki wa asili, utenzi na
kizazi kipya kutoka kwa wasanii nguli jijini hapo. Bonanza hilo lilikuwa na
lengo la kuukaribisha Mwaka 2025 na kuwakaribisha watumishi wote waliohamia Halmashauri
ya Jiji la Dodoma na kuwaaga wastaafu wote chini ya kaulimbiu isemayo “Halmashauri ya Jiji la Dodoma 2025,
Ushirikiano na Umoja Wetu Ndio Nyenzo ya Huduma Bora”.
MWISHO
Comments
Post a Comment