Ofisi ya Rais Ikulu haishikiki kuvuta Kamba
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu kuvuta Kamba
(wanaume) imeibuka na ushindi wa alama 2-0 dhidi ya Timu ya Ofisi ya Rais Jiji
Dodoma kuvuta Kamba (wanaume) katika upande wa wanawake Timu ya Ofisi ya Rais
Ikulu ikiibuka na ushindi wa alama 2-0 dhidi Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma
katika mchezo huo.
Mchezo huo ulifanyika ndani ya Uwanja wa Jamhuri katika Bonanza la Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililohusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, michezo ya jadi na tamasha la sanaa.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo,
Utamaduni na Sanaa Jiji la Dodoma, Patrick Moshi, aliwataka washiriki wa
michezo mbalimbali kujiamini zaidi wawapo uwanjani ikiwa ni njia kufanikiwa na
kupata ushindi katika michezo yao. “Siri ni kufanya mazoezi mapema na wakati
wa mchezo ni kujiamini zaidi na hiyo ndio siri ya mafanikio” alisema Moshi.
Mwamuzi wa mchezo wa kuvuta kamba, Idrisa
Shabani aliwaomba washiriki wa michezo mbalimbali kuwa na tabia ya kufanya
mazoezi mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kukabiriana ipasavyo pindi
wanapokuwa kwenye michuano na timu pinzani. “Watu waje kufanya mazoezi, kama
tunavyoona Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu ilikuwa imejipanga kwa kufanya mazoezi
lakini Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma ilikuwa haijajipanga na ndio maana
wamefungwa” alisema Shabani.
Akizungumzia kuhusu mchezo huo wa kuvuta
kamba, mmoja kati ya washiriki kutoka Timu ya Ofisi ya Rais Jiji Dodoma, Devotha
Selufara, alisema amefurahishwa na kuwepo kwa michuano hiyo na kuomba michezo
hiyo iwe endelevu ili kuendelea kuimarisha afya kimwili na kiakili. “Ninaomba
zoezi hili lisiishie hapa, lijirudie ili tuwe tunafanya mazoezi mara kwa mara
kwasababu ina imarisha viungo vyetu lakini pia afya zetu zinakuwa salama” alisema
Selufara.
Nae, shabiki na mpenzi wa mchezo wa kuvuta
kamba, Perpetua Mtega, aliwaasa washiriki wa michezo mbalimbali kutokuwa na
tabia ya kukata tamaa hasa pale wanapopoteza katika michuano hiyo kwasababu
katika mchezo wowote lazima apatikane mshindi na asiyekubari kushindwa siyo
mshindani. “Nimefurahi kwa sababu wachezaji wote wamejiamini, wamejitoa na
walikuwa tayari kupokea ushindi hivyo sina budi kusema kwamba popote kunapokuwa
na ushindani lazima apatikane mshindi mmoja” alisema Mtega.
Ushindi wa wachezaji katika michezo
mbalimbali hutegemea sana maandalizi mazuri ya awali, uthubutu, kujiamini na
bidii ya kutosha ili kuepuka kuteteleka ndani ya mchezo.
Comments
Post a Comment