Waganga Wafawidhi wa Jiji la Dodoma wapatiwa mafunzo ya Mfumo wa NeST
Na. Halima Majidi, DODOMA
Waganga wafawidhi kaitka Halmashauri ya
Jiji la Dodoma wamewezeshwa mafunzo ya ununuzi kwa njia ya mfumo serikalini ‘National e- Procurement System of Tanzania’
(NeST) yatakayoongeza ufanisi na kurahisisha utendaji wa kazi pamoja na
kupunguza hoja za ukaguzi kwa sababu kila kitu kitakuwa kipo wazi.
Mafunzo hayo yalitolewa na Kitengo cha
Manunuzi na Ugavi cha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa lengo la kuongeza
ufanisi, kupunguza gharama pamoja na kuokoa muda, ambayo yalifanyika katika Ukumbi
wa Shule ya Sekondari Umonga.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Josephat Nyumayo,
alieleza kuwa, mafunzo hayo yalikuwa yanahusu matumizi ya mfumo wa ‘NeST’ katika ngazi ya kata kwa mujibu
wa Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2023 na Kanuni zake za Mwaka 2024, ikiwa ni utekelezaji
wa agizo la serikali kuwa manunuzi yote yafanyike kwa mfumo huo.
Aidha, Nyumayo alisema kuwa, mafunzo
hayo ni ya awamu ya pili kwa waganga wafawidhi ambapo mafunzo ya awali yalikuwa
yanahusu matumizi sahihi ya mfumo wa ‘NeST’
na leo wameongeza kipengele cha uundaji wa kamati ambazo zimeleta mabadiliko
kulingana na muongozo pamoja na sheria mpya. “Mwanzo kulikuwa na kamati tatu
ambazo ni kamati ya ujenzi, manunuzi na mapokezi kwa mujibu wa sheria iliyofanyiwa
marekebisho na muongozo uliotoka unahusisha kamati mbili, kamati tendaji na
kamati ya mapokezi na majukumu ambayo yalikuwa yanafanywa na kamati ya manunuzi
yatafanywa na Afisa Manunuzi alierasimishwa madaraka hayo” alisema Nyumayo.
Nae, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu,
Azania Silliah, alisema kuwa anamshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa kuwapatia mafunzo hayo, kwa sababu ameweza kutumia mfumo huo kwa
kufanya manunuzi na kutoa tuzo kwa wale ambao wameomba ili waweze kupatiwa
mahitaji.
“Kwahiyo, nawashauri waganga wafawidhi
wenzangu na watu wengine, haya mafunzo ni mazuri, tusiyaogope kwanza ni ya
uwazi pia yanaepusha hoja za ukaguzi maana kila kitu kipo wazi” alishauri
Silliah.
Kwa upande wake, Mtumishi wa Zahanati
ya Chololo, Samwel Karidushi, alisema kuwa, mafunzo ameyapokea vizuri, ataenda
kuwaelekeza na kuwa mwalimu kwa watumishi wenzake ili kurahisisha uagizaji wa vifaa.
“Mfumo huu unalenga kusaidia kupunguza gharama ikiwemo nauli za uagizaji wa
vifaa pamoja na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali katika taasisi” alisema
Karidushi.
Vilevile, Mganga Mfawidhi wa Zahanati
ya Chididimo, Isaka Witiche, alisema kuwa, anamshukuru Mkurugenzi kwa Jiji la
Dodoma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, kwa
kuwapatia mafunzo ya manunuzi kwa njia ya kidigitali na kuahidi kwenda
kuyatekeleza. “Kama tulivyoelekezwa kununua vifaa kwa njia ya kidigitali tutaenda
kuhakikisha tunaleta mabadiliko katika vituo vyetu vya kazi” alisema
Witiche.
MWISHO
Comments
Post a Comment