Elimu Kombaini FC Yailaza na Viatu Sheria Ndogo FC
Na. Mussa Richard, DODOMA
Timu ya Mpira wa Miguu ya Elimu Kombaini
imeishushia kipigo cha mbwa mwizi Timu ya Mpira wa Miguu ya Sheria ndogo FC
baada ya kuichabanga mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Jamhuri
Dodoma ikiwa ni muendelezo wa michezo mbalimbali katika tamasha la kuukaribisha
Mwaka 2025 la CCD Watumishi Bonanza lililoandaliwa na Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma.
Baada ya mchezo kutamatika Nahodha wa timu ya
Elimu Kombaini, Given Alestides, alisema “tumefanikiwa kupata matokeo na
tukiwa kama watu wa elimu tumewafundisha wanasheria jinsi ya kucheza mpira wa
miguu na wameelewa, lakini yote kwa yote tumefurahi kushiriki bonanza hili na
tumekutana wa watu wengi na tumejifunza mambo mengi sana, tunampongeza sana
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa ubunifu huu alioufanya”.
Nae Nahodha wa Timu ya Sheria ndogo, Salumu
Bwenda akatoa sababu zilizowafanya wapoteze mchezo huo kwa idadi kubwa ya
mabao. “Mchezo umeisha na tumepoteza kwa bao 3-1 ni matokeo mabaya lakini
sababu kubwa ni kuwa wachezaji wetu wana maumbo makubwa na umri umeenda pia
ndiyo maana hata magoli mengi tuliyofungwa yalitokana na wapinzani wetu kupiga
mipira mirefu nyuma ya mabeki na kukimbia kwa kasi kuingia kwenye boksi letu,
yote kwa yote naamini watu wote wamefurahia mpira kwasababu hii ilikua ni burudani
na ni moja ya mazoezi” alisema Bwenda.
Bonanza hilo lililoandaliwa lilikuwa na lengo
la kuwakutanisha watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuukaribisha
Mwaka 2025 huku kaulimbiu kwa mwaka huu ikiwa ni ‘Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ushirikiano na Umoja Wetu Ndiyo Nyenzo ya
Huduma Bora’.
MWISHO
Comments
Post a Comment