Elimu Sekondari Jiji yawalaza chali Maafisa Watendaji Mchezo wa Pete
Na. Halima Majidi, DODOMA
Katika mchezo uliovuta hisia za mashabiki
wengi, Timu ya Mchezo wa Pete ya Elimu Sekondari ya Jiji la Dodoma imeibuka
kidedea kwa kuishinda Timu ya Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa Jiji la Dodoma
goli 3-2.
Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ulidhihirisha ushindani mkali kati ya timu hizo mbili.
Mchezo ulianza kwa kasi huku wachezaji wa
Elimu Sekondari wakionesha umahiri wa hali ya juu katika kurusha mpira kwa
haraka na ukabaji imara. Katika robo ya kwanza, timu hiyo iliongoza kwa alama 2
dhidi ya 0 za Maafisa Watendaji.
Kocha wa Timu ya Elimu Sekondari, Mwl. Zainabu
Abdallah, alisema amefanya yake katika kuhakikisha wanachukua ushindi japokuwa
mvua imekuwa kikwazo, na aliwapongeza vijana wake kwa kujituma uwanjani na
kutumia mbinu walizofanyia mazoezi, na pia alisisitiza wachezaji wawe na tabia
ya kufanya mazoezi sio tu mpaka wakti wa michezo au bonanza bali iwe ni tabia
endelevu. “Ushindi huu ni matokeo ya nidhamu, mazoezi makali na mshikamano
wa timu yetu, na mazoezi ni afya tunashukuru Mungu" alisema Mwl.
Abdallah.
Nae Nahodha wa Timu ya Elimu Sekondari,
Tulamwona Kihaka, alisema anashukuru Mungu kwa ushindi wa kishindo japo kuwa
mtanange ulikuwa mgumu. Hivyo, amewasisitiza wachezaji wenzie kuendeleza
ushirikiano. “Nawaasa wachezaji kufanya mazoezi kwa sababu changamoto ni
nyingi ila kwa kifupi tumewafunga Maafisa Watendaji Jiji” alisema Kihaka.
Kwa upande wake, Kocha wa Timu ya Maafisa
Watendaji, Mafuru Buriro, alisema kuwa mechi ilikuwa nzuri licha ya kuwa hali
ya hewa haikuwa vizuri kwa sababu haikuwa rafiki hasa kukimbia. Ushindani
ulikuwepo, hata hivyo, timu yake imejifunza mengi na itaendelea kujiandaa kwa
michezo mingine. “Leo tumepata changamoto ikiwemo mvua, hivyo, tunajipanga
bonanza lijalo Timu ya Elimu Sekondari wajipange” alisema Buriro.
Nahodha, wa Timu ya Maafisa Watendaji, Getruda
Katyega, alisema Mchezo ulikuwa mgumu japo kuwa wamepambana na aliahidi kuwa
watajiandaa kufanya vizuri zaidi awamu ijayo kwa sababu hawakuwa na mazoezi ya
kutosha awamu hii.
Ikiwa ni katika shauku za kuuwaga mwaka 2024
na kuukaribisha mwaka 2025 ambapo Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliandaa
bonanza hilo ambapo ilikuwepo michezo mbalimbali.
MWISHO
Comments
Post a Comment