Kilimo yaigaragaza Ardhi, Bonanza la Watumishi, 2025
Na. Mussa Richard, DODOMA
Timu ya Mpira wa Miguu ya Watumishi wa
Divisheni ya Kilimo Mjini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeibuka kidedea baada
ya kushinda penati 6-5 dhidi ya Timu ya Mpira wa Miguu ya Watumishi wa
Divisheni ya Uendelezaji Makao Makuu.
Penati hizo zilipigwa baada ya kutoshana nguvu katika muda wa kawaida ndipo ikaamuliwa kupigwa mikwaju ya penati na Kilimo kuibuka wababe. Mchezo huo ulivurumishwa katika Kiwanja cha Jamhuri Dodoma kwenye Bonanza la kuukaribisha Mwaka 2025 lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Baada ya mchezo kutamatika Nahodha wa Timu ya
Kilimo FC, Michael Lukumai alisema “toka mchezo unaanza sisi tulikua bora
kuliko wao japo walianza kwa kututangulia mabao yote lakini sisi tukawa bora
kuliko wao, ndiyo maana tukafanikiwa kurudisha mabao yote na kwenye mikwaju ya
penati tukaibuka kidedea, lakini yote kwa yote watumishi wamepata burudani na
imekuwa siku ya kihistoria kwetu sote”.
Nae, Nahodha wa Timu ya Ardhi FC, Godwin
Maselo akaelezea sababu zilizofanya wafungwe huku akiwamwagia sifa wachezaji
wenzake kwa kiwango bora walichoonesha. “Mchezo ulikua mzuri na sisi kama Ardhi
tulicheza vizuri ndiyo maana tulikua tunawatangulia kufunga mabao na wao
wanarudisha, tumekuja kupoteza kwa mikwaju ya penati kwasababu penati hazina
mwenyewe. Bahati imekuwa kwao wameshinda, nawapongeza na kila mtu kafurahi siyo
kwa Timu ya Kilimo tu bali hata watumishi wengine waliohudhuria katika bonanza
hili” alisema Maselo.
Bonanza hilo lililoandaliwa na Halmashauri ya
Jiji la Dodoma lilikuwa na lengo la kuwakutanisha watumishi wote na
kuukaribisha Mwaka 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Halmashauli ya Jiji la Dodoma Ushirikiano na Umoja wetu ndiyo nyenzo ya
huduma bora”.
MWISHO
Comments
Post a Comment