Watumishi Waaswa Mshikamano
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya kazi kwa mshikamano katika kutoa huduma zao
kwa jamii ili kuweza kuiinua halmashari izidi kupanda katika utoaji wa huduma
bora kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata ya
Mtumba, Edward Maboje, alipokuwa akitoa wito katika Bonanza la Watumishi
lililofanyika tarehe 25 Januari, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Mshikamano uliooneshwa leo uendelee
hata katika kutoa huduma kwa jamii kwa ngazi zote. Hili jambo la leo, mkurugenzi
na timu yake wameonesha jambo la kutujali watu wa ngazi zote. Kwahiyo, na mimi
ninawaomba sasa, watumishi na sisi madiwani tufanye kazi kwa mshikamano na kwa
ushirikiano mkubwa ili tuiinue halmshauri yetu izidi kupanda. Mimi nimesema
hili ni jambo jipya kwangu na mimi ni mtu mzima, ni jambo jipya. Pia, Dodoma
hapa ni nyumbani, napafahamu vizuri na wakurugenzi wanapita wengi lakini hiki
kitu kimenigusa na ninawaomba watumishi wa Halmashauri ya Jiji tufanye kazi kwa
mshikamano” alisema Maboje.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Makole, Omary Omary, alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa kuona kuna uhitaji mkubwa wa kuandaa Bonanza la Watumishi ambalo linakutanisha
watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili waweze kufahamiana na
kufurahi pamoja. “Nampongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kuweza
kutambua na kuona namna ya kuandaa bonanza zuri kama hili kwa ajili ya
watumishi pamoja na viongozi mbalimbali ambao wanatoka Jiji la Dodoma. Sambamba
na hilo, katika uwanja huu wa Jamhuri umefurika na umejaa viongozi wengi wa
kutosha na kila kiongozi na mtumishi wa jiji anafurahia bonanza kwasababu kuna
michezo mbalimbali inaendelea hapa. Kwahiyo, nimpongeze kwa kuweza kufanya
jambo zuri kama hili” alipongeza Omary.
Nae, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Ihumwa, Mwl. Daudi Mwakalinga, alisema kuwa, kufanya tathmini ya kukutana mara
moja kwa mwaka inaleta picha nzuri na kuwaweka pamoja watumishi na inazidisha
umoja na mshikamano. “Tamasha limekuwa zuri na mpaka sasahivi ninavyozungumza
watu wengi wamefurahia tamasha hili. Kukutana watumishi mara moja kwa mwaka na
kufanya tathmini ya mambo yote tuliyoyafanya kwa furaha, tukafanya michezo mbalimbali
hii inatuweka pamoja watumishi na inatufanya tuonekane kwamba tunapendana na
tunajenga nyumba moja. Nia kuu ya watumishi ni kuhakikisha jiji linasonga mbele
na maendeleo ya taifa yanapatikana kwa umoja wetu kwa kila sekta” alisema
Mwl. Mwakalinga.
Aidha, alishauri kuwa, Bonanza hilo
lisiwe la mwisho bali likawe mwanzo wa mabonanza mengine katika Jiji la Dodoma
ili kuweza kuimarisha mahusiano mazuri baina ya watumishi wote wa Halmashauri
ya Jji la Dodoma.
Hata hivyo, Afisa Utamaduni katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Desdery Kuzenza, aliwashukuru washiriki wote
waliohudhuria Bonanza la Watumishi kwa kuwakumbusha kuwa, bonanza hilo ilikuwa
ni ishara ya kufungua Mwaka Mpya 2025 na kuwasisitiza kutekeleza dhima na dira
ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.
Kuzenza alisema “nitumie fursa hii
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Menejimenti kwa ujumla kuwashukuru
washiriki wote wa Bonanza. Bonanza hili ni ishara ya kuanza mwaka mpya katika
maono ambayo yamejielekeza kupeleka huduma kwa wananchi na wakazi wa Dodoma
sambamba na kutekeleza dira na dhima za Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili
kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora, za uhakika na zinazokidhi malengo ya
walengwa wetu ambao ni wananchi”.
MWISHO
Comments
Post a Comment