Msalala DC watembelea Jiji la Dodoma kujifunza ukusanyaji Mapato

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Madiwani na Wataalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala wamefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujifunza mbinu mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato ili kutekeleza miradi ya maendeleo.


Akiwasilisha taarifa ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato, Mhasibu wa Mapato wa Jiji la Dodoma, Julius Shinji katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, alisema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, halmashauri ilijiwekea lengo la kukusanya jumla ya shilingi 71.675,239,000 kutokana na vyanzo vya ndani. Alisema kuwa hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2026, halmashauri ilikuwa imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 61,328,048,214.71, sawa na asilimia 85.56 ya lengo la makisio ya mwaka.

“Ukusanyaji wa mapato unafanyika kupitia mfumo wa kanda. Halmashauri tumeunda kanda saba za utoaji huduma zenye wataalamu kutoka divisheni na vitengo mbalimbali kupitia ukusanyaji wa moja kwa moja na kwa kudhibiti mianya ya upotevu. Makisio ya mapato kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 ni shilingi 83,860,029,000” alisema Shinji.

Nae, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alieleza kuwa mgawanyo wa kanda ulizingatia mahitaji ya haraka ya huduma pamoja na idadi ya watu katika maeneo husika. Pia alibainisha kuwa katika kanda hizo si ukusanyaji wa mapato pekee unaofanyika bali pia utoaji wa huduma nyingine mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mibako Mabubu alisema kuwa ziara yao katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imelenga kujifunza mbinu na utendaji wa ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa kanda, kutokana na sifa na mafanikio ambayo jiji hilo limekuwa likipata.

Ziara hiyo imewawezesha madiwani na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kupata uelewa mpana kuhusu namna Halmashauri ya Jiji la Dodoma inavyosimamia na kuongeza mapato kupitia mfumo ya kanda.

MWISHO

 

 

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026