Msalala DC wajifunza mbinu za ukusanyaji mapato kupitia mfumo wa kanda Dodoma Jiji
Na. Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imetembelea Ofisi ya utoaji
huduma Kanda Namba Moja iliyopo Soko la wazi la Machinga, Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, ili kujifunza mbinu za ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa kanda
ambao umesaidia kuongeza ufanisi wa makusanyo na kuboresha utoaji wa huduma kwa
wananchi.
Akielezea namna ya utendaji kazi wa kanda hiyo, Nicholaus
Mitembo, Meneja wa Kanda Namba Moja, alisema kuwa kanda hiyo inatoa elimu kwa
wananchi na wafanyabiashara na kuwahamasisha kulipa mapato kwa hiari na kwa
wakati ili kuepuka adhabu na pia kuchangia maendeleo ya eneo lao. Aidha, alisema
kanda hiyo inatarajia kukusanya mapato ya shilingi 19,162,421,314.32.
Nae, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Rose
Manumba, aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kukubali na kutoa nafasi
ya kujifunza katika halmashauri hiyo. Aidha, aliwakaribisha viongozi na
watumishi wa jiji hilo kutembelea Msalala kwa ajili ya kujifunza zaidi kuhusu
shughuli kuu za kiuchumi za eneo hilo, ambazo ni uchimbaji madini na kilimo.
Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala,
Kidana Milando, alisema kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa kujifunza mbinu
mbalimbali zitakazosaidia kuongeza bajeti ya halmashauri kutoka shilingi
bilioni saba hadi bilioni tisa, hususan kutoka maeneo yanayofanya vizuri ndani
ya kanda, ili kupata uzoefu na maarifa yatakayosaidia kuboresha utendaji na
utekelezaji wa majukumu katika halmashauri yao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwalugulu, Halmashauri
ya Wilaya ya Msalala, Frola Sagasaga, alisema kuwa walifika kwa lengo la
kujifunza kuhusu masuala ya ukusanyaji wa mapato. Alifafanua kuwa mwenyekiti
wao aliwashauri kutembelea Jiji la Dodoma kutokana na mafanikio yake katika
ukusanyaji wa mapato kupitia kanda, akibainisha kuwa jiji hilo linafanya vizuri
zaidi katika eneo hilo.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa imewapa madiwani na wataalamu
wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala uzoefu na maarifa mapya yatakayowasaidia
kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kwa lengo la kuongeza ufanisi na
kufikia malengo ya bajeti ya halmashauri yao.
MWISHO
Comments
Post a Comment