Jiji la Dodoma latumia Mil. 29 miundombinu S/M Ihumwa B

Na. Mwandishi Wetu, IHUMWA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa kiasi cha shilingi 29,000,000 kwaajili ya umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa ya Shule ya Msingi Ihumwa B, hatua inayosaidia kuimarisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.




Hayo aliyasema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihumwa B, Mwl. Daudi Mwakalinga wakati alipokuwa akisoma taarifa mbele ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Alisema kuwa fedha hizo zilipeleka mabadiliko chanya shuleni hapo. “Kupitia fedha hizi, shule imefanikiwa kuboresha madarasa, hali iliyochangia kuongeza hamasa kwa walimu na wanafunzi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji” alisema Mwl. Mwakalinga.

Pia, alitoa shukrani kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule. “Tunatoa shukrani za dhati kwa uongozi Jiji kwa kutupatia fedha hizi ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo katika shule yetu. Mazingira ya sasa ni rafiki zaidi kwa walimu na wanafunzi” alishukuru Mwl. Mwakalinga

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya, Joan Mazanda alitoa pongezi kwa uongozi wa shule hiyo, hususan kwa Mwalimu Mkuu kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Usimamizi huu umeonesha matumizi sahihi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika. Pia nipende kusisitiza kuendelea kudumisha uwajibikaji katika miradi ambayo inatekelezwa na serikali” alisema Mazanda.

Fedha za mapato ya ndani zinazotolewa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji zinachangia kuinua kiwango cha elimu katika miradi yote inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma hivyo kuboresha kiwango cha elimu ya mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.






MWISHO

Comments

Popular Posts

Ujenzi wa Darasa Sekondari Anthony Mavunde kupunguza msongamano kwa wanafunzi

Elimu Sekondari Jiji yawalaza chali Maafisa Watendaji Mchezo wa Pete