Odero: Mwenge wa Uhuru alama ya Umoja Wilayani Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Wilaya ya Dodoma wameombwa kuonesha umoja
na mshikamano wao kwa kujitokeza kwa wingi kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru
utakapowasili na kutembelea miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha
yao.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero akionesha utayari wa kuupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2026
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini
kwake kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 katika Wilaya
ya Dodoma.
Alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni chombo cha umoja na mshikamano
ambao umekuwa ukitafsiriwa kwa vitendo wilayani Dodoma. “Wilaya ya Dodoma
tumekuwa tukionesha umoja na mshikamano wa wazi linapokuja suala ya Mwenge wa Uhuru
kwa miaka yote. Hili ni jambo la heshima kwetu. Nitumie nafasi hii kuwaalika na
kuwaomba tena wananchi wote tarehe 1 Juni, 2026 kuupokea Mwenge wa Uhuru katika
Mtaa wa Vikonje B, Kata ya Mtumba na kuukimbiza katika miradi yote ya maendeleo
na kushiriki mkesha mkubwa utakaofanyika katika uwanja Shule ya Msingi Kizota”
alisema Odero.
Mwenge wa Uhuru umekuwa chachu ya kuhamasisha
utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo ‘Tanzania
ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo’ inasadifu lengo la Mwenge
wa Uhuru la kuleta maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Dodoma kwa kuhamasisha
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi. Sisi tunaamini kuwa
maendeleo ni mchakato wa pande zote, hivyo, umoja wetu na mshikamano wetu ndiyo
msingi wa maendeleo yetu” alisema Odero.
Akiongelea falsafa ya Mwenge wa Uhuru alisema kuwa
imejengeka katika misingi ya haki, usawa, umoja na uwajibikaji. “Mwenge
wa Uhuru umetoa mchango mkubwa kwa kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Dodoma,
amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa. Kikubwa zaidi umekuwa
ukihamasisha kupambana na vitendo vya rushwa, uzembe, matumizi mabaya ya
rasilimali za umma” alisema Odero.
Wakati
huohuo, aliwakaribisha vijana wa wilaya ya Dodoma kujitokeza kwa wingi katika
kongamano la vijana. “Mwenge wa Uhuru, utatanguliwa na kongamano ya vijana litakalofanyika
kwa siku mbili tarehe 29-30 Mei, 2026. Kongamano hilo ni fursa kwa vijana
kujifunza mambo mbalimbali kuanzia elimu ya uraia, uzalendo, hadi fursa za
kiuchumi kwa vijana” alisema Odero.
Nae
mkazi wa Wilaya ya Dodoma, Mariam Omary alisema kuwa Mwenge wa Uhuru umekuwa
ukihamasisha umoja na mshikamano kwa wananchi wote kwa sababu unawaunganisha na
kuchochea maendeleo.
MWISHO
Comments
Post a Comment