Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lawafukuza kazi watumishi watatu na mmoja kushushwa cheo
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma
limewafukuza kazi watumishi watatu na mtumishi mmoja kushushwa cheo na mshahara
kufuatia kukiuka misingi na taratibu za Utumishi wa Umma.
Maamuzi hayo yalifanyika katika Mkutano maalum wa Mashauri ya Kinidhamu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Watumishi waliofukuzwa kazi ni Afisa Muuguzi Msaidizi,
Muuguzi na Afisa Mtendaji wa Mtaa. Mtumishi aliyeshushwa cheo na mshahara ni
Mteknolojia Maabara.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Alimwoni Chaula alilihoji Baraza la Madiwani, na kwa kauli moja liliridhia
kuwafukuza kazi watumishi hao watatu na kushushwa cheo na mshahara mtumishi
mmoja.
Akiwasilisha taarifa ya kuhitimisha mashauri ya
nidhamu ya watumishi wanne kwa Baraza maalum la Mashauri ya Nidhamu, Mkuu wa Divisheni
ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, Gerald Ruzika alisema kuwa mkurugenzi aliunda kamati ya uchunguzi kwa
mujibu wa Kanuni ya 45 na 46 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022
kuchunguza tuhuma dhidi ya watumishi wanne.
Akiongelea tuhuma hizo, alisema kuwa watumishi wote,
kamati ilithibitisha tuhuma walizotuhumiwa nazo kuwa ni za kweli isipokuwa
mtumishi wa cheo cha Mteknolojia Maabara ambae kamati haikuthibitisha tuhuma moja
ya kufanya mambo yanayoshusha hadhi ya Utumishi wa Umma kinyume na Kanuni za Utumishi
wa Umma za Mwaka 2022, Kanuni ya 42 Jedwali la kwanza sehemu A (2) kati ya
tuhuma nne alizotuhumiwa nazo.
Akiongelea mashtaka waliyotuhumiwa nayo alisema kuwa Mteknolojia
Maabara alishtakiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa
sababu ya matumizi ya pombe yaliyokithiri, kutumia bila idhini ya mamlaka vifaa
vya umma kwa shughuli zisizohusiana na majukumu yake, kufanya mambo ambayo
yanashusha hadhi ya Utumishi wa Umma, kwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma
na kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano bila kuwa na likizo ama ruhusa ya
mwajiri.
Kwa upande wa Afisa Muuguzi Msaidizi alishtakiwa kwa
kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano bila kuwa likizo au ruhusa ya mwajiri.
Muuguzi alishtakiwa kwa kutokuwepo kazini kwa zaidi ya
siku tano bila kuwa likizo, ruhusa ya mwajiri au sababu za msingi na kutofanya
majukumu aliyopangiwa kama mtumishi wa umma.
Mtendaji wa Mtaa alishtakiwa kwa kutokuwepo kazini
bila kuwa likizo, ruhusa au sababu za msingi na kutotekeleza majukumu
aliyopangiwa kama mtumishi wa umma.
MWISHO
Comments
Post a Comment