WENZA WA VIONGOZI WASHAURIWA KUANZISHA BUSTANI ZA NYUMBANI

Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI

WENZA wa viongozi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kuanzisha bustani za nyumbani ili kusaidia familia zao na wageni wanaowatembelea.

Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Lucy Kway


Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Lucy Kway alipokuwa akiongelea umuhimu wa bustani za nyumbani kwa wenza wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alipokuwa akihamasisha kilimo cha bustani hizo kwenye Banda la Jiji la Dodoma katika viwanja vya Nanenane Nzuguni.

Kway alisema “nichukue nafasi hii kuwashauri wenza wa viongozi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kulima bustani za nyumbani kwa ajili ya kusaidia familia zao na wageni wanaowatembelea. Hii ni muhimu kwa sababu wenza wa viongozi ni mfano wa kuigwa katika jamii hivyo ni rahisi kwa watu kuiga mfano mzuri kutoka kwa wenza wa viongozi hapa Halmashauri ya Jiji la Dodoma”.

Akiongelea kilimo hicho kwa wananchi na watumishi wanaohamia Makao Makuu Dodoma alisema kuwa bustani hizo ni muhimu kwao. Bustani za nyumbani mtu yeyote anaweza kulima kwa muda wowote. Kinachotakiwa ni kulima bustani ndogo inayokuwezesha kujikimu kwa mboga na kuuza. “Kilimo hiki kina faida ya kumpatia mtu kipato. Faida nyingine ni mtu analima mwenyewe na kuondokana na hatari ya kutumia madawa zaidi kwenye mboga. Mtu anaweza kulima na kupata fedha za kujikimu au kuuza” alisema Kway.

Kwa upande wa Mkazi wa Dodoma Leila Shati aliyetembelea banda la halmashauri ya jiji la Dodoma alisema kuwa amevutiwa na kilimo cha bustani za nyumbani. Kilimo hiko ni kama urembo wa nyumbani lakini kina umuhimu mkubwa kwa jamii. “Sisi wakina mama kilimo hiki ni suluhisho la mbogamboga nyumbani kwa sababu unalima eneo dogo kwa mpangilio mzuri na kuwa na uhakika wa mboga” alisema Shati.

Maonesho ya shughuli za wakulima Nanenane mwaka 2023 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.


MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma