Mwalimu Mkuu S/M Mazengo apongezwa usimamizi ukarabati wa shule

Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KASKAZINI

Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imempongeza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo kwa kusimamia vizuri ukarabati wa shule kupitia fedha za mradi wa BOOST na kumtaka kuongeza kasi kukamilisha kabla ya shule kufunguliwa ili wanafunzi wasiwe na upungufu wa madarasa ya kusomea.



Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipoongoza timu hiyo kukagua ukarabati wa shule hiyo jijini Dodoma.

Baada ya kupokea taarifa ya ukarabati wa shule hiyo iliyowasilishwa kwa ustadi na mwalimu mkuu na kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Timu ya Menejimenti alisema kuwa mwalimu mkuu (Mwl. Rehema Nkungu) anafanya kazi kubwa na nzuri ya kusimamia ukarabati wa mradi huo. “Hapa kuna ushirikiano mzuri, ninataarifa ya utendaji mzuri wa (Mkaguzi Majengo, Jacob Stephen) anayesimamia mradi huu tangu nikiwa ofisini, hongera sana. Matamanio yetu, kasi iongezeke ya ukarabati huu ukamilike haraka ili wanafunzi wanapofungua wakute ukarabati umekamilika” alisema Dkt. Sagamiko.

Akielezea utekelezaji wa mradi huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo, Mwl. Rehema Nkungu alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 170,400,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo fedha kutoka mradi wa BOOST. “Shilingi 150,000,000 ni fedha ya ukarabati wa madarasa 13 na shilingi 20,400,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo” alisema Mwl. Nkungu.

Alisema kuwa malengo ya ukarabati huo ni kuboresha miundombinu ya madarasa kwa ajili ya matumizi salama. “Kurejesha ubora wa majengo yaliyoharibika na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma ya elimu kupitia mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia” alisema Mwl. Nkungu.

Shule ya Msingi Mazengo ilianza tarehe 1 Januari, 1970 hadi sasa ina wanafunzi 720, kati yao wavulana ni 324 na wasichana 396.







MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Watumishi wa Kanda Namba Tatu watembelea Zahanati ya Soweto

Gari la Darasa Tembezi latoa elimu Mitaa ya Jiji la Dodoma