Jiji lataka mpango kazi kukamilisha ujenzi shule ya Mil. 299,200,000 utekelezwe

Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imemuagiza Mkuu wa Shule ya Sekondari Nzuguni kusimamia mpango kazi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya mkondo mmoja yenye gharama ya shilingi 299,200,000 fedha kutoka mradi wa BOOST ili ikamilike kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.




Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipoongoza timu hiyo kutembelea na kukagua hatua ya ujenzi wa shule hiyo katika Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma.

Alisema kuwa mpango kazi wa ujenzi wa shule hiyo unatakiwa kufahamika na kila anayehusika na kusimamia utekelezaji wake ili ujenzi ukamilika kwa wakati. Idadi ya mafundi anatakiwa kuongezeka ili kuhakikisha mradi unakamilika haraka, aliongeza.

Pia, ilishauriwa manunuzi yote ya vifaa pamoja na madawati yatangazwe kwenye mfumo wa NeST mapema ili kusiwe na ucheleweshaji katika utekelezaji wa mradi.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa shule mpya ya msingi mkondo mmoja kwa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nzuguni, Mwl. Rogers Justinian alisema kuwa shule ilipokea shilingi 299,200,000 fedha kutoka mradi wa BOOST. Ujenzi unaotekelezwa ni jengo la utawala, madarasa sita ya msingi, madarasa mawili ya awali, matundu 12 ya vyoo vya msingi na matundu sita ya vyoo vya awali, alisema.

Alisema kuwa ujenzi uliganywa katika ‘lots’ sita ili kupata mafundi sita, kwa madarasa mawili kila ‘lot’, jengo la utawala na vyoo. Hatua iliyofikiwa ni upauaji kwa madarasa manne na vyoo, majengo mengine yapo kwenye hatua ya lenta.

Akiongelea matumizi ya fedha alisema kuwa shilingi 125,678,528 zilitumika kulipa wazabuni na mafundi, bakaa ni shilingi 176,521,472.





MWISHO

Comments

Popular Posts

SERIKALI YAPONGEZWA KUTOA FEDHA UJENZI WA DODOMA ENGLISH MEDIUM

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma

Nanenane ni muhimu kujifunza Kilimo na Ufugaji bora