Jiji la Dodoma lataka kasi ukarabati madarasa Kitelela Sec

Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI

TIMU ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeelekeza kuongeza kasi ya ukamilishaji wa ukarabati wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kitelela ili wanafunzi watakapofungua shule mwezi Januari, 2026 waweze kuyatumia.



Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipoongoza timu hiyo kutembelea na kukagua maendeleo ya ukamilishaji wa ukarabati wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kitelela iliyopo Kata ya Nzuguni, jijini Dodoma.

Dkt. Sagamiko ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa baada ya kukagua hali ya ukarabati inavyoendelea, kasi siyo ya kuridhisha. “Hivyo, maelekezo yetu ni kwamba, kasi iongezeke ili mradi ukamilike kwa wakati na shule zinapofunguliwa wanafunzi waanze kutumia madarasa hayo” alisema Dkt. Sagamiko.

Wakati huohuo, alimuagiza Afisa Mtendaji wa Kata ya Nzuguni na Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kitelela kuweka kambi katika mradi huo na kusimamia ratiba ya utekelezaji na kuhakikisha changamoto zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo ya upatikanaji wa maji.

Vilevile, mkuu wa shule aliagizwa kusimamia menejimenti ya vifaa vinavyonunuliwa, kupokelewa na kutolewa kwa ajili ya shughuli za ukarabati na kusisitiza utunzaji sahihi wa kumbukumbu. “Hapa, daftari la mali za serikali au kitabu cha kumbukumbu za mali za serikali lazima kitumike vizuri kuandika orodha ya mali na vifaa vyote vya serikali vinavyonunuliwa kwa ajili ya kazi ya ukarabati” alisema Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Vincent Odero.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukamilishaji wa ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kitelela, Mwl. John Mswelo alisema kuwa shule hiyo ilipokea fedha tarehe 18 Novemba, 2025 kupitia akaunti ya Shule ya Sekondari Nzuguni B kwa ajili ya ukamilishaji wa madarasa mawili na ofisi, ujenzi ulianza tarehe 11 Desemba, 2025.

Akiongelea utekelezaji wa mradi, alisema kuwa kazi zilizofanyika ni upigaji lipu kuta za ndani na nje na ‘blundering’ ndani ya jengo. “Kazi zilizobaki ni ‘blundering’ sehemu ya nje, kufunga bodi katika dari, kupaka rangi, kuweka mfumo wa umeme, uwekaji wa milango na uwekaji wa marumaru katika sakafu. Kiasi cha shilingi 6,865,830 kimetumika kwa ajili ya manunuzi ya vifaa awamu ya kwanza” alisema Mwl. Mswelo.

Awali akiikaribisha Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika eneo la mradi, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Mwl. Fredrick Mwakisambwe alisema kuwa halmashauri ilitoa kiasi cha shilingi 20,7743,095 kwa ajili ya kukamilisha mradi kiporo wa madarasa mawili na ofisi katika Shule ya Sekondari Kitelela.

Shule ya Sekondari Kitelela ipo kilometa 22 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma, ilifunguliwa tarehe 13 Januari, 2025 ikiwa na wanafunzi 31 na inatarajia kupokea wanafunzi 21 wa kidato cha kwanza mwaka 2026.





MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Watumishi wa Kanda Namba Tatu watembelea Zahanati ya Soweto

Gari la Darasa Tembezi latoa elimu Mitaa ya Jiji la Dodoma