Chidachi S/M watakiwa kuboresha mpango kazi wa fundi kukamilisha ujenzi mradi wa BOOST
Na. Dennis Gondwe, MKONZE
Mhandisi wa halmashauri, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Chidachi wametakiwa kufanya mapitio ya mpango kazi wa mafundi na kuandaa mpango
wa haraka unaotekelezeka ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa miundombinu kwa gharama
ya shilingi 182,100,000 fedha kutoka mradi wa BOOST shuleni hapo.
Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipoambatana na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukagua ujenzi wa mradi wa miundombinu katika Shule ya Msingi Chidachi kwa fedha za ufadhili wa BOOST.
Timu ya Menejimenti ilipokagua mradi huo haikuridhika
na kasi ya ujenzi na kuelekeza mhandisi wa halmashauri, mwalimu mkuu pamoja na
fundi kupitia upya mpango kazi na kutengeneza mpango kazi wa haraka
unaotekeleza ili kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Mkurugenzi alisema kuwa kila mmoja anatakiwa kuongeza
umakini katika usimamizi ili mradi ukamilishwe kwa viwango, na kusema kuwa
menejimenti haitachelewesha malipo ya fundi kwa namna yeyote.
Akisisitiza katika utekelezaji wa mradi huo, alisema
kuwa ujenzi wa madarasa uende sambamba na ununuzi wa madawati na ujenzi wa
jengo la utawala uende sambamba na ununuzi wa samani. “Nimesisitiza haya kwa
sababu hakuna fedha itakayoongezwa kwenye mradi huu kwa ajili ya samani”
alisema Dkt. Sagamiko.
Katibu wa Kamati ya Ujenzi, Mwl. Veronica Suya alisema
kuwa shule ilipokea shilingi 182,100,000 kutoka mradi wa BOOST kwa ajili ya
ujenzi wa madarasa mawili ya awali na matundu sita ya vyoo, madarasa mawili ya
elimu msingi na jengo la utawala. “Utekelezaji wa mradi huu ulianza tarehe 23
Septemba, 2025. Mradi unalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha
mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi” alisema Mwl. Suya.
Shule ya Msingi Chidachi ipo katika Mtaa wa Chidachi,
Kata ya Mkonze ilianzishwa tarehe 3 Aprili, 2004. Shule ina wanafunzi 1,717 na
walimu 50.
MWISHO
Comments
Post a Comment