RAIS SAMIA ANAPENDA KUFANYA KAZI NA VIONGOZI WA DINI - DKT. BITEKO
📌 Asisitiza milango ya
Rais Samia ipo wazi kwa ajili ya mazungumzo kwa mustakabali wa Taifa
📌 Asema Serikali
inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Taasisi za dini
📌 Serikali kuendelea
kushirikiana na Taasisi za dini kuchochea maendeleo
📌 Uchaguzi ni daraja la
amani na maendeleo si chanzo cha mifarakano – Baba Askofu Shoo
📌 CCT
yahimiza maadili ya kisiasa, utulivu wa jamii na kampeni za kistaarabu
📌 Taasisi za dini Afrika
zatajwa kuchangia maendeleo ya sekta ya afya kwa 30%- 70%
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini
kwa kuwa anawaongoza wananchi wenye dini ambao dini zao wanaziheshimu na hivyo
asingependa kuona haki zao zinanyimwa kwa namna yoyote ile.
Dkt. Biteko aliyasema hayo jijini
Dodoma wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano
Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
“Mheshimiwa Rais Samia anapenda
kufanya kazi na viongozi wa dini na ninyi ni mashahidi amekuwa akiwaalika ili
tuzungumze masuala mbalimbali ya kitaifa ingekuwa ni mtu anayejifungia ndani na
akasema analo jeshi, sheria, katiba na vyombo vya ulinzi basi nitafanya kazi
nadhani hivi ingekuwa ngumu sana lakini yeye amesema milango yetu iwe wazi
tuzungumze na viongozi wa dini kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa nchi yetu
pale ambapo tunadhani hatuendi sawasawa,” amesema Dkt. Biteko.
Akijibu hoja za CCT, Dkt. Biteko alisema
kuwa imekuwa desturi ya nchi kuwa na waangalizi wa ndani kwenye Uchaguzi Mkuu
na kuwa ni imani yake kuwa Tume Huru ya Uchaguzi itawalika waangalizi wa
ndani ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia. Hata hivyo amesisitiza Tume Huru ya
Uchaguzi iachiwe uhuru wake wa kufanya kazi zake.
Aliwahakikishia kuwa Serikali
inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na taasisi zote za dini ikiwemo
makanisa na kusema kuwa tangu Uhuru mwaka 1961, Taasisi za dini zimeendelea
kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwanufaisha watu wengi kote nchini.
“Tunawapongeza sana na tunawashukuru
sana kwa mchango wenu. Tafiti zinaonesha kuwa Taasisi za dini Barani Afrika
huchangia kati ya asilimia30 hadi 70 ya maendeleo ya sekta ya afya. Kidunia,
kwa mfano katika elimu, Vyuo kama University of Edinburgh - (Scotland), Oxford
University - Uingereza na University of Kwa Zulu - Natal Afrika ya
Kusini vilianzishwa na Taasisi za dini,” alisema Dkt. Biteko.
Aliendelea kuzungumzia mchango wa
taasisi za dini katika kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali duniani ambao
wanaendelea kuiokoa dunia kutoka katika matatizo na majanga mbalimbali akitolea
mfano Taasisi ya World Coucil of Churches na World Vision kwa kutoa huduma
za kibinadamu duniani kote bila kubagua tofauti zilizopo za dini, rangi, kabila
na jinsia.
Katika kutambua mchango wa viongozi
wa dini Afrika na duniani kote, Dkt. Biteko alielezea haiba ya Mwanatheolojia
Muanglikana kutoka Afrika Kusini, Hayati Baba Askofu Desmund MpiloTutu kama
kiongozi wa dini mwenye upendo, mpendahaki na amani, ambaye amechangia kutetea
haki za binadamu na kupambana dhidi ya u baguzi na hivyo kusaidia kuleta
maendeleo na usawa kwa nchi ya Afrika Kusini na dunia kote.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikistro
Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Fredrick Shoo alipongeza usikivu wa Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za Serikali za kudumisha demokrasia kwa
kuruhusu mikutano ya hadhara sambamba utekelezaji wa miradi ya maendeleo
nchini.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025, Baba Askofu Dkt. Shoo alisema kuwa CCT inahimiza maadili ya
kisiasa na utulivu wa jamii ikiwa ni pamoja na kampeni zisizo za kuvunjiana
heshima bali zinazoweka mbele maslahi ya Taifa na kupinga vitendo vyote vya
rushwa.
“Uchaguzi ni daraja la amani na
maendeleo si chanzo cha mifarakano, jamii idumishe amani, mshikamano na
uzalendo wa kila mmoja kwa nafasi yake. Pia Tume Huru ya Uchaguzi iendelee
kusimamia haki kwa kushirikiana na waangalizi wa ndani amesema ,” Baba Askofu
Shoo.
Alibainisha kuwa CCT itaendelea
kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya jamii hivyo ameiomba Serikali itoe
unafuu wa kodi na kutotoza ruzuku kwa misaada inayotolewa na wahisahi ili
kuboresha ubora wa huduma na kuwafikia wananchi.
Katibu wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Mchungaji Dkt. Moses Matonya alisema kuwa CCT ni Jumuiya
inayounganisha madhehebu wanachama 12 na mashirika ya kikristo 14. Aidha,
katika Mkutano huo jumla ya wajumbe waliohudhuria ni 224 kati ya
wajumbe wote 280.
Chanzo: MICHUZI BLOG
Comments
Post a Comment