TANESCO SACCOS YAIGUSA SEKTA YA AFYA KWA KUTOA MASHUKA YENYE THAMANI YA MILIONI 23 JIJINI DODOMA
Na. Janeth Raphael, MichuziTv -Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary
Senyamule amesema pamoja serikali kufanya kazi kubwa hasa katika Sekta ya Afya
ikiwemo ununuzi wa vifaa, Dawa, Majengo na miundombinu na watumishi lakini bado
safari ya maendeleo katika sekta hiyo huwa haiishi kutokana na watu kuongezeka
na magonjwa kubadilika.
RC Senyamule alisema hayo jijini
Dodoma katika hafla fupi ya kupokea Mashuka 300 ya kuhudumia wagonjwa waliopo
katika hospitali za Mkoa wa Dodoma yaliyotolewa na wana Ushirika wa Tanesco
Saccos.
Alisema kuwa kutoka na uhitaji wa
kila siku serikali hata kama ingenunua mashuka mengi kiasi gani bado
yasingeweza kudumu siku zote kwasababu ingefika muda yangechakaa na kuhitajika
mengine.
“Tunajua kuwa serikali yetu chini ya
Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia imefanya kazi kubwa sana katika Sekta ya Afya. Zipo
sekta nyingine lakini katika sekta ya Afya imefanya makubwa kuanzia
Vifaa,Majengo,Miundombinu,Watumishi na vitu vingine vingi, lakini tunafahamu
kuwa bado safari hii ya maendeleo haina mwisho kila siku tunafanya lakini bado
watu wanaongezeka na magonjwa yanabadilika kupelekea uhitaji wa kila siku
katika baadhi ya maeneo. Kwahiyo, mahitaji hayafiki mwisho hata siku moja.
Hivyo, ukienda kwenye sekta ya Afya unakuta kuna uhitaji mpya, mfano mashuka
hata serikali ikinunua mengi kiasi gani lakini baada ya muda yachakaa na
kuhitajika mengine” alisema Senyamule.
Aidha, aliipongeza Tanesco Saccos kwa
mchango huo wa mashuka ambao ni wa thamani na heshima kwa wana Dodoma
utakaowagusa wagonjwa ambao watafika katika Hospitali za Mkoa wa Dodoma ambazo
zitapewa mashuka hayo ambayo yataleta kumbukumbu nzuri, kwasababu fedha
zilizotakiwa kununua mashuka katika hospitali hizo sasa zitakwenda kununua Dawa
na vifaa vingine.
Naye Mtendaji Mkuu wa Tanesco Saccos, Andrea
Hilary alisema kuwa katika zoezi hilo la kutoa mahitaji ya mashuka katika hospitali
walipata msukumo kwa kujua kuwa sekta ya Afya ni kubwa na yenye uhitaji mwingi.
Hivyo, serikali pekee haiwezi kujitosheleza pamoja na kufanya makubwa katika sekta
hiyo, kwasababu uhitaji ni wakila siku na kwa kuona hilo na wao waliona wanayo
nafasi ya kufanya ili kuigusa jamii.
Alisema kuwa walichagua eneo hilo la
kusambaza mashuka baada ya wao kupata elimu kuwa kitanda kimoja kinahitaji
mashuka nane kwa siku ili kukamilisha mzunguko wa mgonjwa kulala katika
mazingira ambayo ni safi na salama. Hivyo, katika mipango yao ya mwaka wakaona
waguse eneo hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanesco
Saccos, Omary Shabani alieleza kuwa wameona ni muhimu kujikita katika sekta ya Afya
ambapo wamechangia mashuka 1,300 katika sekta nzima ya Afya na kwa Mkoa wa
Dodoma wametoa mashuka 300 yenye thamani ya shilingi milioni 23, hiyo yote
ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto zinazoikabiki sekta ya Afya.
Pamoja na kuahidi kuendelea kuifikia mikoa
mingine kwasababu ni awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza walitoa mashuka yenye
thamani ya shilingi milioni 88, mashuka takribani 1,500 na awamu hii ya pili
wameanza na mashuka 1,300.
Mashuka haya yaliyopokelewa na Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma ni Mashuka 300 yenye thamani ya shilingi milioni 23 ambayo
yatagwanywa katika wilaya zote.
Comments
Post a Comment