MAWAKILI NCHINI WATAKIWA KWENDA KUZISOMA SHERIA ZA UCHAGUZI MKUU
Na. Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Mawakili nchini Tanzania wametakiwa kwenda kuzisoma sheria za Uchaguzi Mkuu,
ili waweze kuwasaidia kujaza fomu wagombea waliojitokeza kutia nia, lakini pia
kutatua migogoro itakayowasilishwa kwa kukosa uelewa katika Mahakama mbalimbali
hapa nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania ,George Masaju aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akiwathibitisha na kuwapokea Mawakili 449 wakiwemo wa Serikali na wa kujitegemea, ikiwemo kuorodheshwa rasmi katika orodha ya mawakili waliothibitishwa hapa nchini.
Aidha, aliwataka Mawakili hao kwenda kufanya kazi katika mikoa mingine tofauti
na Dar es Salaam na Dodoma ambayo ina mawakili wa kutosha, ili kuepuka kuitwa
vishoka hasa ukizingatia soko la Kada hiyo ni kubwa kwa sasa.
Alisema kuwa kuna sheria nyingi zikiwemo za Polisi, Uchaguzi na nyingine. Na
kusema kuwa Mawakili wanapaswa kutumia muda mwingi kuzisoma na kuzielewa ili
waweze kutumia fursa ya kuwasaidia wagombea mbalimbali waliojitokeza kuchukua
fomu za kugombea nafasi za uongozi. “Najua kazi zetu nyingi tunazipata kupitia
kutatua migogoro mbalimbali. Hivyo, tuweke jitihada ya kuzisoma sheria ili
tuzielewe maana kuthibitishwa, kupewa vyeti na utendaji ni vitu viwili tofauti”
alisema Jaji Mkuu Masaju.
Vilevile, aliwataka Mawakili kwenda kukiishi kiapo walichoapa na kukifanyia
kazi ipasavyo, wasome sheria kila mara kwa sababu hubadilika, ili waweze
kuisaidia jamii kwa ujumla katika maeneo ambayo watakwenda kuwajibika hapa
nchini. “Sisi tuliojaa hapa wakati mnapewa kiapo hatujaja kuwashangilia tumekuja
kushuhudia kiapo chenu kama mtakwenda kukiishi kama Sheria inavyoelekeza” alisema.
Jaji Mkuu akizungumzia kuhusiana na Mawakili hao kupenda kuishi kwenye miji
mikubwa kama Dar es Salaam na Dodoma, alisema kitendo hicho kinamchukiza sana
kwa sababu kuna maeneo mengi ambayo yana migogoro na kuwataka waende sehemu
hizo wakawatumikie wananchi.
Akitolea mfano Wilaya ya Kilombero ambako kuna mashamba ya miwa, kuna wakulima
wengi pamoja na jamii ambayo inahitaji huduma ya sheria, hivyo, waende huko
kuwatumikia wananchi badala ya kubaki kwenye miji mikubwa. “Nisingependa kuona
mnazunguka Dar es Salaam na Dodoma muonekane kama vishoka, tawanyikeni mikoa
mingine mkafanye kazi ya kutenda haki ili kuisaidia jamii, lakini sitaki
kusikia mnauza utu wenu kwa kupewa fedha badala ya kutenda haki” alisema Jaji
Mkuu.
Alisema kuwa wasitegemee kwenda kuishi kama wanasiasa wao wanapaswa kwenda
kutenda haki ili kuendelea kuaminika mbele ya jamii na kuongeza kuwa kama kesi
haiwezi anapaswa kumwambia mteja wake ukweli na sio kuchukua pesa yake bure. “Msitende
dhambi ya kuchukua fedha ya watu ilihali mnajua kesi huiwezi ni bora umwambie
ukweli mteja, usiwaze kununua gari ndogo kwa pesa ya mteja ambayo unajua kesi
hashindi, hata wewe hutafanikiwa kwa sababu hujui amehangaika vipi kuitafuta
hiyo pesa ili akulipe” alisema.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Chiganga Tengwa alisoma idadi ya
mawakili waliopokelewa na kuthibitishwa huku akiwataka kufuata taratibu
watakazoelekezwa.
Ongezeko la idadi hiyo ya Mawakili waliothibitishwa imefanya kufikia mawakili
13,446 ambao watakuwa wanafanya shughuli za uwakili katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Chanzo: MICHUZI
BLOG
Comments
Post a Comment