MAGEUZI YA ELIMU TANZANIA YAVUTIA NCHI NYINGINE KUJIFUNZA
Mageuzi makubwa yaliyofanyika katika
sekta ya elimu nchini, hususan mafunzo ya Amali yameanza kuvutia mataifa
mengine barani Afrika kuja kujifunza namna yalivyofanyika na utekelezaji wake.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma kufuatia ziara ya Waziri wa Elimu ya Juu, Utafiti, Sayansi na Teknolojia kutoka Jamhuri ya Gambia, Prof. Pierre Gomez ambaye alisema kuwa lengo la kufika Tanzania ni kujifunza mbinu zilizotumika katika kufanya maboresho na maugezi makubwa katika sekta ya elimu.
Waziri huyo alisema kuwa Benki ya
Dunia iliishauri nchi hiyo kuja Tanzania ili kujionea namna utekelezaji wa
Sera, mikakati na miradi mbalimbali katika sekta ya elimu ili kuwawezesha
kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na tija.
“Tumeshuhudia ujenzi wa miundombinu
na mifumo ya mafunzo ya vitendo yenye tija katika vyuo mbalimbali ikiwemo DIT,
VETA na Taasisi, tunaamini kunufaika zaidi kupitia ushikiano katika nyanja
mbalimbali za mafunzo” alisema Prof. Gomez.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania iko tayari
kushirikiana na Gambia katika kubadilishana wakufunzi na wanafunzi ili
kuimarisha uhusiano wa kielimu kati ya nchi hizo mbili.
“Tunaamini kuwa kwa kushirikiana,
tutaweza kuinua viwango vya elimu ya amali barani Afrika na kusaidia vijana
kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Prof. Mkenda.
Ziara hiyo ni ushahidi wa namna
mageuzi ya elimu nchini yanavyotambuliwa kimataifa, na jinsi ambavyo nchi
inavyojenga nafasi yake kama kitovu cha ubunifu na ubora katika elimu ya amali
Afrika.
Chanzo: Blog ya FullShangwe
Comments
Post a Comment