DKT. BITEKO ASEMA TANZANIA INA USALAMA WA CHAKULA, AWAPONGEZA WAKULIMA
* Asema Serikali inatambua Vyama vya Ushirika ni muhimu
kuunganisha nguvu za wananchi na kujiendeleza kiuchumi
* Mauzo ya nje ya kahawa na tumbaku 2023/2024 yaongezeka hadi
Dola za Marekani 19,300,000
* Maono ya Rais Samia yaanza kuonekana sekta ya kilimo
yachangia GDP asilimia 26
* Aziagiza Wizara za Fedha na Kilimo kupata ufumbuzi wa bei
za mazao
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
amewapongeza wakulima nchini kwa jitihada zao za kuzalisha mazao kwa wingi na
hivyo kusaidia nchi kuwa na usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na kuwezesha
sekta ya kilimo kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati akifunga
Kongamano la Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani.
“Leo sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi
yetu, tunazungumza mchango wa GDP wa asilimia 26, tunazungumza mazao ambayo
yanatupa usalama wa chakula katika nchi yetu, nchi zingine zinahangaika kupata
chakula sisi watu wetu wana uhakikia wa kupata chakula mitaani kwa sababu
wakulima wamewezeshwa kufanya biashara ya kilimo” alisema Dkt. Biteko.
Alibainisha kuwa takwimu zinaonesha utendaji wa vyama vya
ushirika umeendelea kuimarika kila wakati mauzo ya nje yameongezeka. Ambapo kwa
mwaka 2024/2025 jumla ya vyama vya ushirika 1,084 viliuza kahawa na tumbaku
moja kwa moja nje ya nchi kiasi cha Dola za Marekani 344,800,000 ikilinganishwa
na Dola za Marekani 325,500,000 kwa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la Dola za
Marekani 19,300,000.
Alifafanua kuwa vyama vilivyopata Hati safi ya Ukaguzi kutoka
Shirika la Ukaguzi la Vyama vya Ushirika (COASCO) vimeongezeka kutoka vyama 339
mwaka 2021/2022 hadi kufikia vyama 631 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la
vyama 292 ambayo ni asilimia 86.13.
Aidha, vyama vilivyopata Hati isiyoridhisha vimepungua kutoka
Vyama 1,198 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Vyama 263 mwaka 2023/2024 sawa na
upungufu wa vyama 935 ambayo ni asilimia 78.
Alitoa rai kwa Vyama kuwawezesha wanawake kwa kuweka mikakati
mbalimbali ili idadi ya Vyama vya Ushirika vya Wanawake iongezeke kutoka Vyama
50 vilivyopo sasa.
Licha ya mafanikio hayo katika sekta ya kilimo, Dkt. Biteko
ameziagiza Wizara za Fedha na Kilimo kupatia ufumbuzi masuala ya bei ya mazao
ya wakulima, pembejeo na mahitaji ya msingi ya wakulima ili kuendelea kufanya
kilimo chenye tija.
“Serikali ya awamu ya Sita inatambua kwamba Ushirika ni
nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika kuunganisha nguvu zao na
kujiendeleza kiuchumi. Hivyo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi na
jitihada zote zenye lengo la kuhakikisha kuwa vyama vya Ushirika vinasonga
mbele kiuchumi na kijamii” amesisitiza Dkt. Biteko.
Alipongeza kuwa vyama vya Ushirika vimekuwa na mchango mkubwa
katika kujenga uchumi wa nchi ndio sababu Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipa
msukumo mkubwa sekta ya kilimo. Pia alimpongeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
kwa kuhakikisha sekta hiyo inatimiza maoni ya Rais Samia ya kuwainua wakulima
kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi.
Vilevile, alimpongeza Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya
Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege kwa kuwasema wakulima nchini na hivyo
kuboresha utendaji kazi wa Vyama vya Ushirika huku akivitaka Vyama hivyo kuwa
na viwanda vya uchakataji wa mazao ili kuongeza thamani ya bidhaa na kuongeza
wigo wa masoko.
Naye, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alimshukuru Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo nchini
ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo, kutoa zuruku za mazao
na kuanzisha kwa Taasisi mbalimbali ikiwemo COPRA zinazolenga kutetea maslahi
ya wakulima nchini.
Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya Serikali
katika maeneo ya vijijini kama vile uwepo wa umeme katika vijiji vyote nchini
na barabara unachochea maendeleo vijijii na hivyo hutoa fursa kwa wakulima
kuanzisha mashine za uchakataji mafuta mfano ya alizeti na kusafirisha mazao
yao.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema kuwa mkoa
huo una vyama vya Ushirika 244 na wananchi wamejua umuhimu wa vyama hivyo
hususan lengo namba saba la kuvitaka kushirikiana na jamii.
Akitoa taarifa ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/23 hadi
2024/25 hali ya vyama vya Ushirika nchini, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika
nchini, Dkt. Benson Ndiege alitaja mafanikio kadhaa yaliyopatika ikiwa ni
pamoja na kuanzisha Benki ya Ushirika katika mikoa minne nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC),
Tito Haule alisema kuwa maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 wanaushirika nchini
wanaungana na wadau wengine duniani hivyo kufanya kuwa maadhimisho ya 102 tangu
kuanzishwa.
Alitaja baadhi ya malengo ya mwaka wa Ushirika 2025 kuwa ni
pamoja na kutoa fursa kwa Vyama Vya Ushirika kuonesha bidhaa zao kwa jamii na
kuhabarisha umma juu ya mchango wa Vyama hivyo na kuhimiza uwepo wa sera na
desturi.
Aidha, alisema baadhi ya mafanikio ya vyama vya Ushirika
nchini ni ongezeko la idadi ya wanachama kutoka milioni 6.9 mwaka 2021/22 hadi kufikia
milioni 10, kuongeza ajira za kudumu na mikataba kwa vijana na kuchangia pato
la kodi kwa Serikali hadi shilingi bilioni 9.5 mwaka 2020/22 na shilingi
bilioni 12.5 mwaka 2023.
Pia, ameishukuru Serikali kwa kuongeza mtaji wa shilingi
bilioni 5 katika Benki ya Ushirika na kuimarisha Vyama Vya Ushirika kwa
kuongeza matumizi ya TEHAMA.
Chanzo: Blog ya Fullshangwe
Comments
Post a Comment