Vijana watakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi

Na. Leah Mabalwe, MNADANI

Mwakilishi wa Kampuni ya MAINLAND inayojenga Kiwanda cha kutengeneza mafuta ya Alizeti, Fadhili Makenjula awataka vijana kujitokeza katika nafasi za kazi mbalimbali zitakazotangazwa na kiwanda hicho cha Mafuta kitakapo kamilika mwezi Juni, 2025 ili kujikwamua kiuchumi.


Mwakilishi wa Kampuni ya MAINLAND inayojenga Kiwanda cha kutengeneza mafuta ya Alizeti, Fadhili Makenjula

Aliyazungumza hayo kwenye Kongamano la Vijana katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 lililofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbwanga jijini Dodoma.

Alisema kuwa vijana wanapaswa kuchangamkia fursa bila kuchagua kazi ili kujikwamua kiuchumi. “Nipende kuwataarifu kuwa, tupo katika hatua ya umaliziaji wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mafuta ya alizeti kilichopo Kata ya Msalato, Mtaa wa Veyula. Vijana jitokezeni kwa wingi katika kutuma maombi ya kazi, kuna vitengo mbalimbali katika kiwanda hicho. Wewe kama kijana usiogope kuleta maombi yako kwaajili ya nafasi ya kazi. Tunawapa vijana nafasi kubwa kwasababu nyie ndio wajenzi wa taifa hili” alisema Makenjula.

Kwa upande wake Mhadhiri Ndaki ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo kikuu cha Dodoma, Dkt. Pius Nyamhanga aliwataka vijana kujitokeza na kushiriki katika fursa mbalimbali za kazi zitakazo jitokeza. Alisema kuwa kizazi hiki kimepata bahati ya kushuhudia mageuzi ya kimaendeleo katika sekta zote. “Vijana wote muwe tayari kujitokeza katika fursa za kazi na muwe mstari wa mbele na tayari kufanya kazi kwa mazingira yanayowazunguka. Fursa nyingi huwa zinatokea mlipo na mara nyingi fursa hizo zinawalenga hasa vijana kama mlivyosikia hapa kuwa kuna nafasi za kazi katika kiwanda kipya cha mafuta ya alizeti. Hivyo, msibaki nyuma na muwe mstari wa mbele kupitia fursa hiyo” alisema Dkt. Nyamhanga.



Alimalizia kwa kusema “niwaombe sana wazazi muwe mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wenu kuzifahamu fursa mbalimbali za kazi. Pia mnawajibu wa kukaa na kuwashauri vijana wenu kutochagua kazi. Mnamchango mkubwa wa kuwapa darasa la maisha vijana wetu hawa” alimalizia Nyamhanga.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri