Mzee Bukitu aongelea Falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwa Vijana Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, MNADANI
Mwenyekiti
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Mzee Joseph Butiku amesema falsafa ya
Mwenge wa Uhuru ilianzishwa kwa lengo la kuleta upendo na mshikamano kwa taifa huku
mwanga wa Mwenge ukiangazia mipaka ili kuleta matumaini palipo kukata tamaa,
upendo palipo uadui na heshima palipo chuki.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Mzee Joseph Butiku akielezea Falsafa ya Mwenge wa Uhuru
Aliyasema
hayo katika Kongamano la Mwenge wa Uhuru la Vijana 2025 lililofanyika katika uwanja
wa Shule ya Msingi Mbwanga. Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 1958 Mwalimu
Nyerere alianzisha falsafa hiyo kipindi cha jitihada za kupata uhuru. “Niwaeleze
kuwa, Mwenge wa Uhuru ni kielelezo cha amani na matumaini. Wakati sisi tunapata
ufahamu kuhusu Mwenge, tuliingiwa na uzalendo wa hali ya juu ndio maana mnaona
taifa letu lipo imara hadi leo” alisema Mzee Butiku.
Aliongeza
kuwa vijana wa kizazi cha leo wanapaswa kuisoma historia ya Mwenge wa Uhuru kwa
mapenzi ya dhati ili kuukuza uzalendo wao na kudumisha amani ya nchi. “Vijana
mlioshiriki kongamano hili nawapongeza sana kwasababu mnajifunza na
kujikumbusha mambo muhimu kwa ajili ya mustakabali wa maisha yenu na ya taifa
letu. Nawasihi muendelee na juhudi hizi na mkawe mabalozi kwa vijana wenzenu
ili kuienzi historia ya Mwenge wa Uhuru kwa uaminifu mkubwa” aliongeza Mzee
Butiku.
Nae Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dodoma Ndaki ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Umma, Justine
Kajerero alisema kuwa falsafa ya mbio za Mwenge wa Uhuru, uadilifu na uongozi vinachochea
uzalendo wa kweli wa kuipenda nchi. “Dhana ya uadilifu ni hali ya kufanya jambo
kwa usahihi hata kama kuna mwanya wa kufanya vingenevyo. Vijana tumeaminiwa
sana na serikali yetu, leo kuwepo mahali hapa kujadili mambo muhimu kama
uadilifu na uongozi ni jambo kubwa litakaloleta matokeo chanya miongoni mwetu”
alisema Kajerero.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Ndaki ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Umma, Justine Kajerero
Aliongeza
kuwa mustakabali wa kuijenga nchi imara yenye vijana waadilifu na viongozi bora
upo mikononi mwa vijana. “Niwaambie kwamba vijana waadilifu wanaandaliwa tangu
sasa, tuhudhurie mijadala ya kujenga ili kuongeza maarifa na uzalendo kwaajili
ya kuuimarisha umoja, upendo na heshima ya nchi yetu” alisisitiza Kajerero.
Katika
hatua nyingine, mwananchi wa Kata ya Mnadani, Julius Mtemi alisema kuwa
amefurahi kushiriki kongamano hilo na amejifunza mambo mengi ikiwemo umuhimu wa
Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mzee Joseph Butiku. “Kiukweli leo nimepata maarifa
mengi, yamenijenga na natumaini nitaenda kuwaeleza jamaa zangu ili nao wajue
umuhimu wa mwenge na uzalendo wa kweli” alisema Mtemi.
Kongamano
la Mwenge wa Uhuru la Vijana Mwaka 2025 ni la pili kufanyika katika Wilaya ya
Dodoma na limewakutanisha vijana 950 waliojadili fursa za kiuchumi kwa vijana,
masuala ya afya na afya ya uzazi na makuzi ya vijana, uongozi, uadilifu,
uzalendo kwa taifa na falsafa ya mbio za Mwenge wa Uhuru, kushiriki Uchaguzi Mkuu
wa Mwaka 2025 kwa amani na utulivu na stadi za kazi na stadi za maisha kwa
vijana.
MWISHO
Comments
Post a Comment