Shekimweri awapa maua yao Vijana Wilaya ya Dodoma

Na. Mussa Richard. DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj. Jabir Shekimweri amewapongeza vijana walioshiriki katika Kongamano la Mwenge wa Uhuru la vijana 2025 lililofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbwanga jijini Dodoma.




Aliyasema hayo wakati akimkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ussi wakati wa kufunga Kongamano la Mwenge wa Uhuru la vijana. “Nimefarijika kuona vijana wamejitokeza kwa wingi na kushiriki ipasavyo katika mada mbalimbali ambazo zimewasilishwa na watoa mada pamoja na wachombeza mada. Pia niwatoe wasiwasi vijana wote walioshiriki katika kongamano hili kuwa mapendekezo yao nimeyapokea na nitayafanyia kazi ili kuhakikisha vijana katika Wilaya ya Dodoma wanajikwamua kimaisha kwa kutatuliwa kwa baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili alisema Alhaj. Shekimweri.

Katika hatua nyingine aliwapongeza watoa mada na wachombeza mada wote walioshiriki katika kutoa mada na mafunzo mbalimbali kwa vijana katika kongamano hilo. “Nitoe pongezi zangu za dhati kwa wataalam na wadau walioshiriki katika kutoa mada na mafunzo yenye tija kwa vijana, mafunzo haya yanaenda kuongeza fikra chanya kwa vijana hawa na wakifuata maelekezo mliyowapatia basi wataenda kufaidika na kongamano hili” alipongeza Alhaj. Shekimweri.

Nae, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025, Ismail Ussi, aliwashukuru vijana wa Jiji la Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo, hali ambayo inaonesha ni kwa namna gani wamekuwa wazalendo kwa nchi yao. “Kwanza kabisa nitoe pongezi kwenu vijana wote mlio itikia wito kwa kushiriki kongamano hili. Hali hii imethibitisha ni kwa namna gani mna uzalendo kwa Mwenge wetu wa uhuru na taifa kwa ujumla. Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zina kaulimbiu inayosema “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu kauli mbiu hii tuibebe sisi kama vijana na tukaifanyie kazi kwa kuwa wahamasishaji wakuu wa amani na utulivu kwenye nchi yetu kabla na baada ya uchaguzi mkuu” alisema Ussi.



Kongamano la Mwenge wa Uhuru la Vijana 2025 Wilaya ya Dodoma lilifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbwanga na kuhudhuriwa na vijana 950, wanaume wakiwa 500 na wanawake wakiwa 450.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi

RC Dodoma apongeza wafugaji kwa ushiriki wa Paredi ya Mifugo

Vijana waalikwa kushiriki Kongamano S/M Mbwanga