Mwenge wa Uhuru waridhishwa na ujenzi wa Barabara yenye urefu wa KM 1.6 kiwango cha lami

Na. Dennis Gondwe, NALA

MWENGE wa Uhuru Mwaka 2025 umeridhishwa na kiwango cha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 1.6 kwa kiwango cha lami kutoka barabara iendayo Singida hadi Hospitali ya Jiji la Dodoma inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.8.



Kauli hiyo ilitolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mwaka 2025, Ismail Ussi alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Nala na maeneo ya jirani waliojitokeza kwa wingi kuupokea na kuushangilia Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 uliotembelea ujenzi wa barabara hiyo.

Alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni ishara ya matumaini, upendo, heshima, amani na maendeleo chini ya serikali ya awamu ya sita. “Leo tumekuja kujionea ujenzi wa barabara ya kisasa yenye ubora, inayojengwa na serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kilometa 1.6 kwa kiwango cha lami. Wananchi wa kata waliomba barabara hii kupitia mbunge na diwani wao. Barabara hii itasaidia wananchi wanapoenda kupata huduma za afya katika Hospitali ya Jiji la Dodoma. Rais, ameendelea kudumisha falsafa ya Mwenge wa Uhuru ya maendeleo, upendo na furaha. Kupitia Mwenge huu unaohamasisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu” alisema Ussi.

Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 1.6 kwa kiwango cha lami kutoka barabara iendayo Singida hadi Hospitali ya Jiji kwa kiwango cha lami kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mwaka 2025, Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Jiji la Dodoma, Mhandisi Ally Bella alisema kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu.



Alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuleta urahisi kwa wananchi kufika katika Hospitali ya Jiji wakati wowote kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za afya. ”Mradi huu wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami unatekelezwa kwa siku 270 kuanzia tarehe 27 Novemba, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Agosti, 2025. Mradi unatekelezwa na mkandarasi mzawa ambaye ni M/S Kings Builders Limited kwa Mkataba Na. 7205/2023/2024/W/22 wenye thamani ya shilingi bilioni 2.8 bila VAT” alisema Mhandisi Bella.

Kuhusu mafanikio ya mradi, aliyataja kuwa ni kurahisisha kufikika kwa huduma za afya kwa kuwezesha wananchi kutoka maeneo mbalimbali kufika kirahisi kupata huduma. Mengine ni kuchochea muamko wa ukuaji wa kiuchumi kwa wananchi katika eneo la Nala na kurahisisha usafiri wa watumishi wanaofanya kazi katika Hospitali ya Jiji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alisema kuwa tangu Wilaya ya Dodoma ianzishwe haikuwa na Hospitali ya Wilaya. Alisema kuwa wananchi wa Kata ya Nala na maeneo ya jirani walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Kanda Benjamini Mkapa. ”Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujibu changamoto za wananchi wa Dodoma, anajenga hospitali kubwa ya Jiji. Na leo tunashuhudia ujenzi wa barabara hii ili kurahisisha mawasiliano kutoka Barabara ya Dodoma-Singida na kuelekea Hospitali ya Jiji” alisema Mavunde.




MWISHO

Comments

Popular Posts

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini – Dkt. Biteko

JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU

WENZA WA VIONGOZI WASHAURIWA KUANZISHA BUSTANI ZA NYUMBANI