Wilaya ya Dodoma mtekelezaji kinara Agenda ya Nishati safi ya kupikia
Na. Dennis Gondwe, NALA
WILAYA ya Dodoma imekuwa ikitekeleza maagizo na
falsafa ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo katika utekelezaji wa dhamira
yake ya nishati safi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alipokuwa akisalimia mamia ya wananchi wa Jiji la Dodoma waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru ulipotembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Santhome - SABS kutembelea mradi wa nishati safi ya kupikia.
Mavunde alisema kuwa Wilaya ya Dodoma ipo
mstari wa mbele kutekeleza maagizo na falsafa ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa vitendo ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi. ”Mheshimiwa mkuu wa wilaya
ninakushukuru sana kwa kusimamia kikamilifu na kuhakikisha taasisi na shule
mbalimbali zinafunga mfumo wa nishati safi ya kupikia. Ndugu Kiongozi wa Mbio
za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mwaka 2025, Wilaya ya Dodoma ni kati ya wilaya kielelezo
kwa nchi yetu katika kutekeleza falsafa ya rais wetu” alisema Mavunde.
Akisoma taarifa ya mradi wa nishati safi ya
kupikia Shule ya Sekondari ya Wasichana Santhome - SABS kwa Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru kitaifa Mwaka 2025, Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Michael
Venancy alisema kuwa lengo la mradi huo ni
kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha wanatumia
nishati safi ya kupikia ili kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya kuni na
mkaa. ”Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 14 Juni, 2024 na ulikamilika tarehe
31 Julai, 2024 na kuanza kutumika. Kazi zilizofanyika ni pamoja na kununua
mitungi na kuweka miundombinu ya uendeshaji wake. Sambamba na hilo tunatumia ’Units
200 KW’ kutengeneza vitafunwa kwa ajili ya wanafunzi kupitia bekari yetu
tuliyonayo hapa shuleni. Vilevile,
tunatumia nishati ya jua kama nishati mbadala endapo ikitokea kuna changamoto
ya umeme” alisema Venancy.
Akiongelea mafanikio ya mradi huo, alisema kuwa umepunguza kuzalisha hewa chafu itokanayo na matumizi ya mkaa na kuni. “Mradi huu umesaidia kuweka mazingira ya usafi. Pia umerahisisha utendaji wa kazi kwasababu matumizi ya nishati hizi yanatumia muda mfupi kukamilisha jukumu lengwa. Kupitia nishati ya jua tumekuwa na uhakika wa nishati hata kipindi ambacho kuna shida ya umeme” alisema Venancy.
Shule ya Sekondari ya Wasichana Santhome - SABS ilianzishwa mwaka
2021 kwa Kidato cha Tano na Sita ikiwa na wanafunzi 56. Mwaka 2024 shule
ilianza elimu ya sekondari ya chini ikitumia shilingi 21,462,000 hadi kukamilika kwa mradi wa nishati safi ya
kupikia na fedha hizi zimetokana na malipo ya ada.
MWISHO
Comments
Post a Comment