Mwenge wa Uhuru kutembelea miradi 7 ya shilingi Bil. 11.1 Dodoma
Na. Dennis Gondwe, CHIGONGWE
MWENGE
wa Uhuru Mwaka 2025 utatembelea miradi saba ya maendeleo yenye gharama ya
shilingi bilioni 11.1 iliyotekelezwa kwa ajili ya kuwapelekea maendeleo na
kuboresha maisha ya wananchi katika Wilaya ya Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri (kushoto) wakati akipokea Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Bahi
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri wakati akipokea
Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Bahi tukio lililofanyika
katika uwanja wa Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Chigongwe jijini Dodoma.
Shekimweri
alisema kuwa Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 ukiwa katika Wilaya ya Dodoma
utachochea maendeleo. “Mimi Jabir Mussa Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,
nakiri kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mheshimiwa
Joachim Nyingo ukiwa unawaka, unang’aa na unameremeta. Aidha, nakiri kuwapokea
wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa wakiwa na afya njema. Mwenge wa Uhuru ukiwa
katika Wilaya ya Dodoma, utakimbizwa umbali wa kilometa 70.6, utatembelea
miradi ya maendeleo saba yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 11.1”
alisema Shekimweri.
Awali
akitoa taarifa fupi ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 kwa Wilaya ya Bahi, Mkuu wa
Wilaya hiyo, Joachim Nyingo alisema kuwa wilaya yake ilifanikisha Mbio za
Mwenge wa Uhuru salama. Alisema kuwa Mwenge wa Uhuru wilayani Bahi ulikimbizwa
umbali wa kilometa 164, ulitembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi miradi
sita yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1.5.
Akiongelea msisitizo wa Mwenge wa Uhuru wilayani kwake alisema kuwa ni ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Msisitizo mwingine aliutaja kuwa ni matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kutunza mazingira na uzalendo katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
MWISHO
Comments
Post a Comment