Madiwani Jiji la Dodoma washauriwa kutafsiri miradi ya maendeleo kwa wananchi
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa
kutafsiri kwa vitendo maana ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika
kubadilisha maisha ya watu na kuyafanya kuwa bora kuliko jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza
la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati
akifungua mkutano wa Baraza la Madiwani wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji
kutoka kwenye kata kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili-Juni, 2024) uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Prof. Mwamfupe ambae pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma alisema “hakuna ubishi wowote jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyopeleka fedha nyingi za kutekeleza
miradi ya maendeleo katika maeneo mengi ya Jiji la Dodoma. Penye ubishi ni pale
tunaposhindwa kutafsiri miradi hii kwenye maisha ya watu ya kila siku. Lazima
tuongelee jinsi mwananchi wa kawaida alivyosaidika na miradi hii. Mfano, treni
ya SGR ilikuwa ni ndoto, lakini juzi ilivyozinduliwa ilikuwa ni halisi. Kazi yetu
wanasiasa ni kuelezea mwananchi anavyonufaika”.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji
la Dodoma, Wendo Kutusha alitoa shukrani kwa halmashauri kutekeleza miradi
mingi ya maendeleo. Aidha, alishauri ushirikiano baina ya Divisheni ya elimu na
watendaji wa kata katika kudhibiti utoro wa wanafunzi katika baadhi ya maeneo
ili kuongeza ufaulu.
Wakati huohuo, Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Asma Karama aliishukuru serikali kwa kutoa fedha nyingi Jiji la Dodoma. “Napenda
kumshukuru Mheshimima Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa jicho la
huruma na kutupatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo” alisema Karama.
MWISHO
Comments
Post a Comment