Shule ya Viziwi Dodoma yapokea msaada wa matendo ya huruma

Na. Emanuel Charles, DODOMA

Shule ya Viziwi Dodoma yakabidhiwa msaada wa mahitaji muhimu ya kijamii yenye thamani ya shilingi 2,00,000 ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma yaliyoandaliwa na Dodoma Jiji Day kwa lengo la kuhimiza upendo, ushirikiano na mshikamano.



Msaada huo ulikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri katika shule hiyo iliyopo Kisasa jijini Dodoma ambapo alikabidhi mchele, sukari, vifaa vya usafi na taulo za kike.

Alisema kuwa ipo thawabu ya utoaji na kuwajali watu wenye mahitaji maalum. “Kutoa siyo utajiri, ni moyo. Japokuwa tulichotoa kinaweza kuonekana kidogo kwa namna moja ama nyingine, lakini naamini kitaenda kuwasaidia watoto hawa, hasa katika kupata chakula shuleni na kuboresha mazingira yao ya kujifunzia” alisema Alhaj Shekimweri.

Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mpango wake wa kuibadilisha shule hiyo kuwa ya mchanganyiko ili kuwaunganisha watoto wenye mahitaji maalumu ya usikivu na wale wasio na changamoto, hatua itakayoongeza ujumuishwaji na weledi kwa pande zote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Dodoma, Charity Sichona alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya muendelezo wa matendo ya huruma kufuatia sherehe ya kuuaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka 2026. “Tuliona ni muhimu watoto hawa nao kujihisi ni sehemu ya sherehe za jiji letu, ndiyo maana tukaandaa bajeti ya shilingi 2,000,000 kwa ajili ya kununua mahitaji haya na kuwakumbuka” alisema Sichona.

Nae, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Viziwi Dodoma, Mwl. Awadhi Mbogo aliipongeza serikali kwa kuendelea kuiunga mkono shule hiyo. Tunaishukuru sana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jiji la Dodoma, mbali na mahitaji tuliyopokea leo, tumekuwa tukipokea shilingi 5,000,000 kila mwezi kwaajili ya kuwahudumia watoto wenye changamoto ya usikivu. Huu umekuwa msaada mkubwa katika kuboresha lishe na mazingira yao ya kujifunzia” alisema Mwl. Mbogo.








MWISHO

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa ujio wa Bandari Kavu Ihumwa