Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa ujio wa Bandari Kavu Ihumwa

Na. Nancy Kivuyo, DODOMA

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula apongeza Mkakati wa Uendelezaji Bandari Kavu na kuahidi kujipanga kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanapata fursa ya kufanya biashara katika eneo hilo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.




Akizungumza katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwenye Bandari Kavu Ihumwa iliyokuwa na lengo la kujiridhisha na mkakati wa uendelezaji wa miundombinu hiyo, alisema kuwa uongozi wa jiji utakaa kikao na kutathmini namna ya kuandaa mazingira rafiki ya biashara ili kuwawezesha wajasiriamali wa ndani kushiriki kikamilifu katika shughuli za upokeaji, uhifadhi na usafirishaji wa mizigo.

Alieleza kuwa pamoja na fursa za moja kwa moja zitakazotokana na shughuli za bandari hiyo, jiji pia linatarajia kuimarisha sekta ya usafirishaji, uhudumu na biashara ndogondogo hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.

Aidha, Mstahiki Meya Chaula aliongeza kuwa jiji litafanya utaratibu wa kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ili kuweka utaratibu mzuri wa usafiri wa kufika katika Bandari Kavu na kurejea katikati ya jiji. Alisisitiza kuwa mpango huo utasaidia kupunguza changamoto za usafiri kwa wafanyabiashara na wananchi pamoja na kurahisisha mzunguko wa bidhaa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ardhi na Majengo kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kokwika Ishenkumba alieleza kuwa wapo kwenye mazungumzo na Jiji la Dodoma ya kupata hati ya eneo hilo ili kurasimisha ardhi na kuweza kuitumia kikamilifu kama ambavyo wamekusidia ili kuleta tija kiuchumi. “Tupo kwenye mazungumzo na Jiji la Dodoma, tuna imani kuwa tutafanikiwa kupata hati ili tuweze kutumia eneo letu sasa kikamilifu kufanya miradi ambayo tumeazimia tukizingatia ushauri wa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuelekea ujio wa AFCON mwaka 2027” alisema Ishenkumba.





MWISHO

Comments

Popular Posts

Shule ya Viziwi Dodoma yapokea msaada wa matendo ya huruma