Wanawake waaswa kupaza sauti unyanyasaji wa Kijinsia
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Wanawake na wasichana waaswa kutoa taarifa za
unyanyasaji wa kijinsia kwa wakati pindi wanapofanyiwa ukatili huo.
Hayo yalisemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Dawati la Kisheria, Rehema Mwalyambi wakati alipotembelea Kituo cha Redio A FM, wakati wa ziara ya wanawake wa Jiji la Dodoma katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni shamrashamra kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho yake kitaifa yatafanyika mkoani Arusha.
Mwalyambi alisema “wanawake wote pamoja na watoto wa
kike tunaomba msiogope kutoa taarifa katika dawati la kijinsia lilipo
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwasababu tunaona wanawake
wengi wanaogopa sana kutoa taarifa pale wanapofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.
Naomba sana msiogope kwasababu sasa hivi kuna haki kwa kila mtu awe mwanamke au
mwanaume, kuna sheria na adhabu pia pale tuu mtu atakapofanyiwa vitendo ukatili.
Sisi kama dawati la msaada wa kisheria tupo kwaajili ya kutoa msaada kwa
wanawake wote wanaofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia”.
Nae, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Joyce Shija aliwatoa hofu wanawake na watoto kuhusiana na ukatili wa
kijinsia, na kuwaahidi kuwa, endapo utatendeka ukatili wa kijinsia watapatiwa
wanasheria kwaajili ya kufuatilia na kusimamia kesi zao.
“Niwatoe hofu wanaoogopa kutoa taarifa pindi
wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia gharama. Dawati la
maendeleo ya jamii linatoa huduma bure kwa kila mmoja na kila mtanzania ana haki
ya kupata haki sawa. Hivyo basi, sisi tumejipanga vema kwaajili ya kukomesha
unyanyasaji, kwahiyo wanawake wote tusiwe nyuma kupata haki zetu inabidi
tupambanie kwasababu hivi sasa ni usawa kwa kila mmoja awe mwanaume au mwanamke
tunahaki sawa” alisema Shija.
Siku ya Wanawake Duniani rasmi ilianzishwa tarehe 8 Machi
1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia siku hii kutumika kuikumbusha Dunia juu
ya haki za wanawake kwa lengo la kuongeza chachu katika harakati za mapambano
ya usawa kwa mwanamke katika jamii. Maadhimisho hayo mwaka huu kitaifa
yatafanyika mkoani Arusha yakiwa na kaulimbiu “Wanawake na Wasichana 2025:
tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji”.
Habari hii imehaririwa na Faraja Mbise
MWISHO
Comments
Post a Comment