Jiji latoa 25,000,000 kumalizia Bweni Mbalawala Sec

Na. Nancy Kivuyo, NALA

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yatoa shilingi 25,000,000 kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa bweni kwa Shule ya Sekondari Nala kwa lengo la kuwaondolea wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule na kuongeza ufaulu.


Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Fredrick Mwakisambwe alipokuwa akisoma taarifa ya umaliziaji wa bweni, vyoo na utengenezaji wa vitanda katika Shule ya Sekondari Nala kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma.

Mwl. Mwakisambwe alisema “shule hii ilianza rasmi tarehe 05 Aprili, 2005 ikiwa na wanafunzi 71. Idadi ya wanafunzi iliendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na shule kukumbwa na changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni wanafunzi wengi kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani. Hata hivyo, changamoto hiyo ilikuwa kubwa zaidi kwa wanafunzi wa kike na hivyo, uongozi wa shule pamoja na bodi waliomba kujengewa mabweni kwaajili ya wanafunzi wa kike kwa lengo la kuwaepusha na changamoto ya kukatisha masomo lakini pia kupandisha ufaulu wao na shule kwaujumla.

Alisema kuwa mwishoni mwa mwaka 2023 shule hiyo ilipokea fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kiasi cha shilingi 25,000,000 kwa awamu mbili kwaajili ya umaliziaji wa bweni moja lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 48, vyoo matundu manne na utengenezaji wa vitanda 25 ambavyo ni double deka za chuma. Fedha hiyo iliingizwa katika akaunti ya shule tarehe 23 Agosti, 2023 kiasi cha shilingi 15,000,000 na tarehe 20 Septemba, 2023 kiasi cha shilingi 10,000,000… Katika kutekeleza na kusimamia mradi huu, mfumo wa ‘force account ulitumika kufanya malipo ya wazabuni. Pia, mkuu wa shule aliunda kamati tatu, ambazo ni kamati ya ujenzi, kamati ya manunuzi na kamati ya mapokezi na ukaguzi. Aidha, utengenezaji wa vitanda 25 ulifanyika na kugharimu jumla ya shilingi 5,000,000.00 tu. Kazi hizi zote zilifanyika na kukamilika kwa gharama ya fedha ya shilingi 21,458,500 ambapo malipo ya wazabuni yalikuwa shilingi 18,008,500, malipo ya fundi shilingi 3,090,000 na gharama za maji shilimgi 360,000. Aidha, kiasi cha shilingi 3,541,500 kilibaki kama salio baada ya kukamilika kwa kazi hizo. Kutokana na changamoto kubwa ya maji hapa shuleni, kamati iliamua kutumia kiasi hiki tajwa kuchimba na kujenga karo kubwa lenye ujazo wa lita elfu 25 kwaajili ya kuhifadhia maji, ununuzi wa simtank moja la lita 5000 na kufunga gata za kuvunia maji ya mvua” alisema Mwl. Mwakisambwe.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Bilioni 9.1 yanufaisha vikundi kwa Mwaka 2020-2023

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma