Jiji latoa Mil 20 kukuza mtaji Kikundi cha Winning Star
Na. Faraja Mbise, IPAGALA
HALMASHAURI ya Jiji la
Dodoma ilikipatia mkopo usio na riba wa shilingi 20,000,000 Kikundi cha Winning
Star kwa ajili ya kuongeza mtaji kwa shughuli ya ufugaji kuku wa mayai na nyama
na kuongeza wigo wa ajira.
Kauli hiyo ilitolewa na
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga
wakati akisoma taarifa ya Kikundi cha Winning Star kinachojishughulisha na
ufugaji wa kuku wa mayai na nyama katika Kata ya Ipagala mbele ya kamati ya
Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma ilitotembelea kikundi hicho.
Sebyiga alisema “lengo kuu la kikundi hiki ni kutumia fursa ya ufugaji ili kuajiri na kutoa ajira kwa wengine hasa vijana. Aidha,
kujikwamua kiuchumi kwasababu kwa
kufanya hivyo, kikundi kimeondoa utegemezi na umasiki kwenye familia hupungua.
Matamanio ya kikundi ni kufuga kuku 10,000 kutokana na uhitaji mkubwa wa mayai
hapa Dodoma”.
Akiongelea mtaji wa
kikundi hicho, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Jiji huyo alisema kuwa mtaji wa
kikundi hicho ulitokana na michango ya wanakikundi pamoja na mkopo wa
halmashauri. “Kikundi kilianza
kwa mtaji wa shilingi 6,300,000, kila mwanachama alichangia kiasi cha shilingi 1,050,000 ambazo zilipatikana kutokana na kuweka
fedha kwenye vikoba. Kikundi kilianza kwa kununua kuku 500, ambapo kwa kipindi cha miaka miwili mtaji ulikuwa
hadi kufikia 31,250,000. kwa kuwa na kuku 2,500 kabla ya mkopo. Halmashauri
iliwapatia mkopo wa asilimia nne kiasi cha shilingi 20,000,000 kutoka mfuko wa wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu tarehe
30
Machi, 2023. kiasi hicho
kimesaidia kuongeza kuku 1,000 pamoja na ‘cage’
za kisasa za kuku, hivyo,
kufikia kuku 3,500” alisema Sebyiga.
Kuhusu
mafanikio ya kikundi, aliyataja kuwa ni kuweza kujilipa posha ya asilimia 30 ya mapato ya kila
mwezi kutokana na mauzo ya mayai na mbolea. “Kikundi kimefanikiwa kuajiri vijana wa kiume
watatu na mama mmoja. Wanakikundi
wamefanikiwa kutimiza ndoto yao ya kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine. Kikundi kimefanikiwa kutoa mafunzo ya ufugaji kwa
wanaokuja kukitembelea na kuongeza
mabanda kwaajili ya kuku wengine” alisema Sebyiga.
Kikundi cha wanawake cha Winning Star,
kilipo Mtaa wa Ilazo Mbuyuni, Kata
ya Ipagala kilianzishwa tarehe 12 Desemba, 2020 kikiwa na wanachama sita.
Kikundi kinajishughulisha na ufugaji wa kuku wa Mayai na Nyama, kimesajiliwa na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma
tarehe 8 Septemba, 2022 na kati ya mkopo wa
shilingi 20,000,000 kimefanikiwa kurejesha shilingi 14,000,000 na kubakiza
shilingi 6,000,000 zitakazolipwa zote kufikia mwezi Juni, 2025.
MWISHO
Comments
Post a Comment