Jiji la Dodoma linafursa lukuki uwekezaji
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma inazo fursa lukuli kwa ajili ya wawekezaji na wafanyabiashara
katika maeneo ya kilimo, viwanda, biashara, michezo na maeneo mengine
yanayoweza kusisimua ukuaji wa uchumi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdul Chacha alipokuwa akizungumza na wajumbe wa
Mkutano wa Baraza la Biashara Wilaya ya Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba. “Halmashauri
ya Jiji la Dodoma ina fursa nyingi sana, una fursa ya kuwekeza katika maeneo ya
michezo kwa ujumla, kwasababu saizi tunaangalia AFCON inakuja. Kwahiyo, watu
wengi watahitaji sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya michezo. Vilevile, nyumba
za kupanga na kuuza (apartments). Kipindi hiki wageni wanaingia wengi sana
hivyo, wanahitaji sehemu za kufikia kwa maana ya malazi, hizo ni fursa
zinazopatina. Lakini biashara mbalimbali za chakula kama kuku, nyama,
mbogamboga na matunda ni mahitaji katika soko la Jiji la Dodoma. Sasa hivi,
mtaona magari mengi ambayo yalikuwa yanatoka mikoani yanaenda Dar-es-Salaam
yanashusha bidhaa zao hapa Dodoma. Kwahiyo, hata mzunguko wa pesa umeongezeka
mara dufu tofauti na ilivyokuwa zamani” alisema Chacha.
Akiongelea
utatuzi wa changamoto, alisema kuwa baraza hilo limekuwa msaada mkubwa. “Changamoto
nyingi tumeweza kuzitatua. Mfano, wafanyabiashara wanalalamika kuhusu ushuru au
kodi zilizowekwa ambazo hawazifahamu, lakini baada ya kukutana nao katika vikao
vyetu, tunawafahamisha zile kodi zimewekwa kwa utaratibu gani, malengo yake ni
yapi. Wafanyabiashara wamekuwa wakielewa na utaratibu unaendelea. Pia
changamoto nyingine tuna wafanyabiashara wadogo na wa kati, wafanyabiashara
wadogo mfano machinga wanachangamoto ya maeneo ya kufanyia biashara. Hivyo,
tunakaa nao na kuongea na kukubaliana mambo ya msingi. Baraza hili kupitia
halmashauri wataandaliwa maeneo maalumu ambayo utaona wanapewa yakiwa na huduma
zote za msingi ili waweze kutoa huduma zao” aliongeza Chacha.
Akiongelea
ujio wa reli ya kisasa (SGR) alisema kuwa imesaidia kukuza biashara katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma. “Kitakwimu bado tunaendelea kufanya tafiti zetu, lakini
kiwango kikubwa sana mtaona ‘movement’ ya watu kwenda Dar-es-Salaam na kurudi
ni kubwa zaidi. Hii imefanya biashara katika Jiji la Dodoma isiwe na tofauti
kubwa na ile iliyopo katika Jiji la Dar-es-Salaam kwasababu zinapatikana kwa
wepesi na gharama nafuu kwasababu wafanyabiashara hawatumii muda mrefu sana
kufuata bidhaa zao” alisisitiza Chacha.
Kaimu
mkuu huyo wa Divisheni ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara aliwataka wafanyabiashara
na watanzania kwa ujumla kulipa kodi kwa uaminifu ili kuleta maendeleo katika
nchi. “Tumeendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha watanzania kwa ujumla kwamba
kodi zao ndio zinazojenga nchi, upatikanaji wa kodi zao ndio unaofanya
maendeleo yote yanayoonekana sasahivi yanatokana na kodi zao. SGR ni kodi zao, miundombinu,
barabara, huduma za kijamii, huduma za afya zote zinaweza kufanyika kwasababu
ya kodi zao. Kwahiyo, mchango wa kodi ya wananchi ni muhimu sana kwa maendeleo”
alisisitiza Chacha.
Nae
mkazi wa Kikuyu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jema Wenslaus alisema kuwa ujio
wa treni ya SGR umeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Alisema kuwa awali alikuwa
akipanga safari ya kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam na kuipangua kutokana na muda
wa kusafiri kuwa mrefu. “Baada ya kuanza kwa SGR sasa unaweza kwenda na kurudi
siku hiyohiyo tena bila kuchoka. Treni hii hakika inaokoa muda na imerahisisha
maisha” alisema Wenslaus.
Baraza
la Biashara la Wilaya ya Dodoma linahusisha wafanyabiashara kutoka sekta ya
umma na sekta binafsi kwa lengo la kujadili masuala ya biashara na uwekezaji
kwa mapana, changamoto na utatuzi wake, muelekeo na namna ya kufikia maelengo ya
halmashauri, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
MWISHO
Comments
Post a Comment