Fursa uwekezaji kilimo cha Zabibu Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kivutio
kikubwa katika kilimo cha zabibu nchini kutokana na zao hilo la kibiashara
kustawi vizuri na kuwanufaisha wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni
ya Kilimo mjini Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi alipokuwa alielezea fursa za kilimo
zinazopatikana Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Mkutano wa Baraza la Biashara
Wilaya ya Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Munishi aliwashauri wawekezaji na
wakulima kuwekeza katika kilimo. “Zipo fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo
mengi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Tuna fursa kubwa ya uwekezaji kwenye kilimo
cha zao la Zabibu. Zao la Zabibu inalimwa hapa Dodoma kwahiyo, mtu yeyote
anaweza akatumia fursa hiyo kwa kuangalia maeneo yale yenye uwezekano mkubwa wa
kulima zao hilo, ambayo yapo maeneo ya Hombolo Bwawani, Makulu, Chihanga, Matumbulu,
Mpunguzi na Mbabala. Kwahiyo, tunaangalia ule mnyororo mzima wa zao la Zabibu,
jinsi ambavyo unaweza kutengeneza ‘wine’, juisi na matunda” alisema Munishi.
Akiongelea uwekezaji wa halmashauri
katika kilimo hicho alisema kuwa imewekeza kwa kiwango kikubwa kwa kuboresha
zao hilo liwe la kibiashara.
“Halmashauri ya Jiji imewekeza katika
kilimo hiki kwa sababu imefundisha wataalam na wengine kupelekwa nchini Afrika
ya Kusini kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kuboresha kilimo cha Zabibu. Kwahiyo,
ni fursa ambayo mtanzania na mwanadodoma unakaribishwa kuwekeza kwenye mnyororo
wa thamani wa zao la Zabibu” alisema Munishi.
MWISHO
Comments
Post a Comment