Jiji la Dodoma linafursa lukuki uwekezaji
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma inazo fursa lukuli kwa ajili ya wawekezaji na wafanyabiashara
katika maeneo ya kilimo, viwanda, biashara, michezo na maeneo mengine
yanayoweza kusisimua ukuaji wa uchumi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu wa Baraza la Biashara la Wilaya ya Dodoma, Abdul
Chacha alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Biashara Wilaya
ya Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
uliopo Mji wa Serikali Mtumba. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina fursa nyingi
sana, una fursa ya kuwekeza katika maeneo ya michezo kwa ujumla, kwasababu
saizi tunaangalia AFCON inakuja. Kwahiyo, watu wengi watahitaji sehemu ambazo
zimeandaliwa kwa ajili ya michezo. Vilevile, nyumba za kupanga na kuuza
(apartment). Kipindi hiki wageni wanaingia wengi sana hivyo, wanahitaji sehemu
za kufikia kwa maana ya malazi, hizo ni fursa zinazopatina. Lakini biashara
mbalimbali za chakula kama kuku, nyama, mbogamboga na matunda ni mahitaji
katika soko la Jiji la Dodoma. Sasa hivi, mtaona magari mengi ambayo yalikuwa
yanatoka mikoani yanaenda Dar-es-Salaam yanashusha bidhaa zao hapa Dodoma. Kwahiyo,
hata mzunguko wa pesa umeongezeka mara dufu tofauti na ilivyokuwa zamani”
alisema Chacha.
Akiongelea
utatuzi wa changamoto, alisema kuwa baraza hilo limekuwa msaada mkubwa. “Changamoto
nyingi tumeweza kuzitatua. Mfano, wafanyabiashara wanalalamika kuhusu ushuru au
kodi zilizowekwa ambazo hawazifahamu, lakini baada ya kukutana nao katika vikao
vyetu, tunawafahamisha zile kodi zimewekwa kwa utaratibu gani, malengo yake ni
yapi. Wafanyabiashara wamekuwa wakielewa na utaratibu unaendelea. Pia
changamoto nyingine tuna wafanyabiashara wadogo na wa kati, wafanyabiashara
wadogo mfano machinga wanachangamoto ya maeneo ya kufanyia biashara. Hivyo,
tunakaa nao na kuongea na kukubaliana mambo ya msingi. Baraza hili kupitia
halmashauri wataandaliwa maeneo maalumu ambayo utaona wanapewa yakiwa na huduma
zote za msingi ili waweze kutoa huduma zao” aliongeza Chacha.
Akiongelea
ujio wa reli ya kisasa (SGR) alisema kuwa imesaidia kukuza biashara katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma. “Kitakwimu bado tunaendelea kufanya tafiti zetu, lakini
kiwango kikubwa sana mtaona ‘movement’ ya watu kwenda Dar-es-Salaam na kurudi
ni kubwa zaidi. Hii imefanya biashara katika Jiji la Dodoma isiwe na tofauti
kubwa na ile iliyopo katika Jiji la Dar-es-Salaam kwasababu zinapatikana kwa
wepesi na gharama nafuu kwasababu wafanyabiashara hawatumii muda mrefu sana
kufuata bidhaa zao” alisisitiza Chacha.
Mkuu
huyo wa Divisheni ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara aliwataka wafanyabiashara
na watanzania kwa ujumla kulipa kodi kwa uaminifu ili kuleta maendeleo katika
nchi. “Tumeendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha watanzania kwa ujumla kwamba
kodi zao ndio zinazojenga nchi, upatikanaji wa kodi zao ndio unaofanya
maendeleo yote yanayoonekana sasahivi yanatokana na kodi zao. SGR ni kodi zao,
miundombinu, barabara, huduma za kijamii, huduma za afya zote zinaweza
kufanyika kwasababu ya kodi zao. Kwahiyo, mchango wa kodi ya wananchi ni muhimu
sana kwa maendeleo” alisisitiza Chacha.
Baraza
la Biashara la Wilaya ya Dodoma linahusisha wafanyabiashara kutoka sekta ya
umma na sekta binafsi kwa lengo la kujadili masuala ya biashara na uwekezaji
kwa mapana, changamoto na utatuzi wake, muelekeo na namna ya kufikia maelengo ya
halmashauri, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
MWISHO
Comments
Post a Comment