Makamu wa Rais azungumza na viongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma
MJUMBE wa
Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa
wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Serikali ngazi ya
Mkoa wa Dodoma kuendelea kutafutia ufumbuzi migogoro ya ardhi iliyokithiri
hususan fidia kwa ardhi iliyotwaliwa na utekelezaji wa mgawanyo wa ardhi wa 70%
kwa 30%.
Makamu wa
Rais ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na Viongozi na Wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma katika Mkutano uliyofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema changamoto hiyo ya ardhi
mkoani Dodoma kwa kiasi kikubwa imewafanya wanachama pamoja na wananchi
kuwa na manung’uniko na hata kufikia hatua ya kususia uchaguzi. Amemuagiza Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma kushirikiana na Waziri wa Ardhi kwa pamoja na uongozi
wa Jiji la Dodoma kuongeza nguvu zaidi katika kushughulikia migogoro hiyo.
Dkt. Mpango
amewahimiza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Dodoma kusimamia miradi na
mapato ya Chama kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mali za CCM
zinatumika kwa manufaa ya Chama ili kuimarisha uchumi na kuepuka kuathiri
uendeshaji wa shughuli za Chama hicho. Aidha amewasihi kusimamia vema na
kuhimiza ulipaji wa ada za uanachama suala ambalo ni muhimu na la kikatiba.
Makamu wa
Rais amewataka wanachama na viongozi wa CCM mkoani Dodoma kuhakikisha hali ya
utulivu inakuwepo katika chama kwa kuendelea kutekeleza vema majukumu katika
ngazi zote, kufuata Kanuni na Taratibu zote, kufanya vikao kwa kuzingatia
Katiba ya Chama na kalenda ya vikao, kuondosha mivutano yoyote baina ya
Viongozi au Viongozi na Wanachama inayotishia ustawi wa Chama
hicho.
Halikadhalika
amewaagiza viongozi na wanachama kuepuka siasa za makundi na migogoro ndani ya
chama. Amesema ni muhimu kufanya maamuzi yahusuyo chama kupitia vikao halali na
kuwasihi kufanya vikao katika ngazi za mashina, matawi, kata, Wilaya na
Mkoa pamoja na kuendesha semina za mafunzo ya itikadi ya chama.
Pia ametoa
rai kwa viongozi wa CCM wa ngazi zote kudumisha ushirikiano na kuendeleza
uhusiano mzuri wa kikazi na Watendaji wa Serikali kwa kufanya kazi kwa karibu
ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025 kwa kuzitafutia ufumbuzi kero
mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Awali
akimkaribisha Makamu wa Rais na Mlezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amesema Chama cha Mapinduzi mkoani humo kimeendelea
kujiweka karibu na wananchi kwa kusikiliza na kutatua kero zao ambapo katika
changamoto ya migogoro ya ardhi kwa kipindi cha mwezi Januari – Julai 2024
jumla ya watu 674 walitatuliwa migogoro yao na chama hicho.
Kimbisa
ameongeza kwamba Chama kimeendelea kutoa mafunzo ya itikadi, kuhamasisha
ulipaji wa ada za wanachama pamoja na kuingiza wanachama wapya kwa kuwasajili
katika mfumo wa kielekrotiniki.
Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mkoa huo umeendelea kutatua kero mbalimbali
za wananchi ambao kwa kipindi cha miaka mitatu jumla ya kero zaidi ya 26,000
zimetatulia huku kero zaidi ya 4000 zikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Amesema kwa sasa mkoa huo umeingia katika mfumo maalum kutoka Ofisi ya Rais
Utumishi na Utawala Bora unaowawezesha wananchi wa Mkoa wa Dodoma wanauwezo wa
kutuma kero zao katika mfumo huo na kutatuliwa.
Mkutano huo
umehudhuriwa na Viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi kutoka kata 209 za mkoa wa
Dodoma, Wabunge, Madiwani, Machifu, Wazee wa Mkoa wa Dodoma pamoja na
Wanachama.
Imetolewa na
Ofisi ya
Makamu wa Rais
16 Agosti, 2024
Dodoma
Comments
Post a Comment