Diwani Fundikira adhamiria kumaliza Kero za Wafanyabiashara wa Soko la Mavunde
Na. John Masanja, CHANG’OMBE
Diwani wa Kata ya Chang'ombe, Bakari Fundikira
amefanya kikao na viongozi wa Soko la Mavunde chenye dhamira ya kuziangazia
changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo na kuzifanyia
utatuzi.
Diwani wa Kata ya Chang'ombe, Bakari Fundikira akiongea na waandishi wa habari
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Ofisi ya Kata ya Chang'ombe iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kikao
hicho, Diwani Fundikira alisema moja ya changamoto walizozitambua ni pamoja na changamoto
ya uwelewa wa mikataba pia kutozingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa
shughuli za kibiashara ndani ya soko.
“Lengo letu sisi viongozi ni kuhakikisha kuna
uelewa mzuri kwa wafanyabiashara hawa kuhusu jinsi ya kuendesha shughuli zao
wakiwa kwenye mazingira rafiki kwa kuzingatia sheria na taratibu. Pia serikali
yetu iweze kukusanya mapato pasipo mtu kushurutishwa wala kulazimishwa” alisema
Diwani Fundikira.
Aidha, alitoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea
kutunza mazingira na miundombinu ya soko ili iweze kudumu kwa muda mrefu na
kuwataka wasisite kujitokeza pale inapoitishwa mikutano yenye kujadili masuala
mbalimbali ya maendeleo hususani utatuzi wa changamoto wanazokumbana nazo.
Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Erick Matiku alisema kuwa wafanyabiashara wengi wa Soko la
Mavunde wamekuwa na changamoto ya utafsiri wa mikataba yao hali inayowapelekea
kuingia kwenye migogoro isiyo ya lazima. Aliahidi kuendelea kutoa elimu zaidi
kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Chang’ombe katika
kuondokana na changamoto hizo.
Wakati huohuo, Mtunza Fedha wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko la Mavunde, Elizabeth Boniface alisema kuwa amekuwa akiwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi za Halmashauri kwa wakati.
MWISHO
Comments
Post a Comment