JIJI LA DODOMA LAPONGENZWA KLINIKI YA ARDHI ILIYOWATOA WATAALAM OFISINI KUHUDUMIA WANANCHI
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuanzisha Kliniki ya Ardhi iliyowafanya
wataalam kutoka ofisini na kuweka kambi kuwahudumia wananchi eneo moja ikiwa ni
utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akiongea na waandishi wa habari katika Kliniki ya Ardhi jijini Dodoma |
Shekimweri
alisema “kipekee nimpongeze Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, niliyasema haya
wakati tunakupokea hapa Dodoma baada ya kuteuliwa. Mimi nakufahamu unavyofanya
kazi. Ninafahamu ni mtu unaejali sana watu na matatizo ya wananchi. Nilikuwa
nawaambia wananchi ninajua kuna mkurugenzi atawasilikiza kwa nafasi na kwa staa
na atawashughulikia matatizo yenu yaliyowasumbua kwa muda mrefu”.
Alisema
kuwa Rais alishaelekeza wataalam kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kutatua
kero zao. “Haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba tutoke ofisini na kwenda
kushughulikia matatizo ya wananchi. Na hapa Dodoma sekta ya Ardhi ndiyo kero
sugu. Tatizo kubwa lazima lishughulikiwe kwa ukubwa wake. Nimekuja hapa
kukupongeza na kukutia nguvu pamoja na menejimenti, lakini kupongeza utaratibu
huu. Hapa wataalam wote wapo hivyo hakuna kupigana tarehe” alisema Shekimweri.
Mkuu
huyo wa wilaya aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika kliniki
hiyo. “Niwapongeze wananchi wote mliojitokeza kwa wingi siku ya leo. Jana
wananchi zaidi ya 1,000 walijitokeza hii inaonesha mlivyo na imani na serikali
yenu katika kutatua kero zenu. Niwaombe kuendelea kutuamini tuna dhamira ya
dhati kushughulikia matatizo yenu” alisema Shekimweri.
Akiwa
katika kliniki hiyo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma pamoja na mambo mengine alikabidhi
hati miliki saba kwa wananchi zilizoandaliwa muda mfupi uliopita.
Kwa
upande wake mwananchi wa Dodoma mjini, Mwajuma Seja alimshukuru Mungu kwa
kupata hati yake. “Mheshimiwa Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji pia
nawashukuru sana kupata hati yangu. Sipo peke yangu wapo wenzengu 24, mimi peke
yangu ndio nimebahatika kupata Hati wenzangu wote hawajapata hata ‘control
number’ alisema Seja kwa masikitiko.
![]() |
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma katika Kliniki ya Ardhi Jiji la Dodoma |
MWISHO
Comments
Post a Comment