HATI 240 ZATOLEWA SIKU YA KWANZA YA KLINIKI YA ARDHI JIJINI DODOMA

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

SIKU ya kwanza ya utekelezaji wa Kliniki ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yapokea wananchi 1,014 ikitoa Hati miliki 240 baada ya kusikiliza wananchi 514.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo akiongea na waandishi wa habari kuhusu siku tano za Kliniki ya Ardhi katika Jiji la Dodoma


Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu Kliniki ya Ardhi iliyoanza siku ya pili katika jiji hilo kutatua migogoro ya Ardhi.

Kayombo alisema kuwa siku ya jana walipokea wananchi 1,014. “Wananchi tuliofanikiwa kuwasikiliza jana ni 514. Katika wananchi 514 tumefanikiwa kutoa Hati 240. Tulifanikiwa kusikiliza watu wenye migogoro 209. Wale waliobaki jana tumeendelea nao leo asubuhi. Leo watu ni wengi kuliko jana na wameshapewa namba na huduma zinaendelea vizuri” alisema Kayombo.

Akiongelea matarajio ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa ni kutatua migogoro ya Ardhi kwa kiasi kikubwa. “Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wa Dodoma hawalii kwa sababu ya Ardhi. Jambo hili ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais hataki kuona wananchi wa Dodoma wanatoa machozi kwenye Ardhi ndio maana tupo hapa kuwashughulikia wananchi wa Dodoma” alisema Kayombo.

Kwa upande wake mwananchi wa Dodoma mjini, Mwajuma Seja alimshukuru Mungu kwa kupata hati yake. “Mheshimiwa Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji pia nawashukuru sana kupata hati yangu. Sipo peke yangu wapo wenzengu 24, mimi peke yangu ndio nimebahatika kupata Hati wenzangu wote hawajapata hata ‘control number’ alisema Seja kwa masikitiko.

Kliniki ya Ardhi imewaweka pamoja wataalam wote wa sekta ya Ardhi ili kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma