WASIMAMIZI KLINIKI YA ARDHI WATAKIWA KUJALI MAKUNDI MAALUM

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WASIMAMIZI wa Kliniki ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutoa kipaumbele kwa makundi maalum yanapokwenda kupata huduma katika kliniki hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akiongea na waandishi wa habari


Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabr Shekimweri alipokuwa akiongea na waandishi wa habari alipotembelea Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika siku yake ya pili jijini hapa ya kutatua migogoro ya Ardhi.

Shekimweri alisema “niwaombe sana, mkusanyiko huu una watu mchanganyiko wapo wa umri wa kati, watu wazima, wazee, wenye changamoto za malazi, wajawazito na wenye ulemavu. Pamoja na utaratibu uliopangwa tuheshimu mahitaji ya haya makundi maalum” alisema Shekimweri.

Aidha, aliwataka wananchi wanaokwenda kupata huduma katika kliniki hiyo kwenda na nyaraka kamili ili kuwasaidia wataalam katika kutatua kero za ardhi. “Wakati wa kuwasilisha changamoto na kero tujitahidi kuja tukiwa tumekamilisha nyaraka za kuunga mkono hoja tunayoijenga. USipokuwa na nyaraka husika utakuwa umepoteza muda wako, njoo ukiwa umejipanga na nyaraka zako zote ili zitusaidie kukuhudumia” alisema Shekimweri.

Vilevile, aliwataka wataalam kuwahudumua wananchi wa heshima na utu. “Wataalam tuendelee kuwasikiliza wananchi hawa kwa heshima, tutangulize utu na tuwe na kauli nzuri kwa wananchi. Moja ya changamoto kubwa ni kauli zisizofaa kwa wananchi. Ni lazima tutangulize heshima kwenye utendaji kazi wetu” alisisitiza Shekimweri.

Kliniki ya Ardhi imewaweka pamoja wataalam wote wa sekta ya Ardhi ili kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma